Simiyu/Bunda. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewaomba wananchi wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu kumpa ridhaa ya kuendeleza mambo muhimu aliyoanzisha na nia yake ya kuongeza mengine kwa ajili wananchi hao.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 katika Kata ya Lamadi, Busega, akiwa njiani kuelekea mkoani Mara kuendeleza kampeni yake, Samia ametaja sekta za afya, elimu, miundombinu kama maeneo ya kipaumbele na kueleza mengi yaliyofanyika ndani ya miaka mitano ya uongozi wa chama hicho.
“Tunakwenda kuboresha hospitali ya wilaya hii kwa kujenga jengo kubwa na bora la mama na mtoto. Mimi ni mama na nimewekeza nguvu katika kuboresha eneo hili kwa ajili ya kina mama,” amesema mgombea huyo.
Samia amesema CCM ikichaguliwa wataendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vya Veta ili vijana wa Busega wapate mafunzo ya ufundi na kujiajiri na kuajiriwa.

“Kwenye umeme vijiji vyote vimepata umeme, mkitupa ridhaa tunamalizia vitongoji vyote kwa sababu ilani ya CCM ya 2025/30 tumepanga kuwa na viwanda ili kuongeza thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini, umeme utasaidia kuendesha viwanda,” amesema.
Mgombea huyo ameendelea kusema kuwa anaikumbuka ahadi yake ya kujenga soko kuu wilayani hapo, katika eneo la Lamadi na sasa yupo tayari kukamilisha ndoto hiyo pamoja na stendi kuu katika eneo la Nyashimo ili kuendelea kuboresha eneo hilo.
Wananchi waliofika kumsikiliza mgombea huyo katika eneo hilo, wameeleza matumaini walionayo kwa Samia huku kina mama wakieleza namna mradi wa maji utaenda kuwanufaisha.
“Tumekuwa na changamoto ya maji, lakini kwa namna mama Samia ametutendea na sasa anaenda kukamilisha mradi wa maji, tunaamini kuwa changamoto zetu zitaisha. Hatuwezi kubadilisha mawazo kwa haya tunayoyaona amefanya,” amesema Jenifa Bweri, mkazi wa Lamadi.
Naye Yusuf Hussein, mfanyabiashara wa saluni, amesema umeme haukatiki tena na vijiji vyote vimefikiwa, hivyo biashara yake ni ya uhakika kwa sasa na inamsaidia kuhudumia familia yake.
“Nimeamua kuwa na ofisi nyumbani kwangu, maana ni karibu na mjini kwa sababu umeme wa kutosha upo. Barabara zetu, hospitali na maboresho katika sekta ya elimu, yote haya yanatufanya tuendelee na Samia kwa kumpa kura nyingi.
“Tumejiandaa kushiriki uchaguzi kwa amani ili tupate wawakilishi wa nafasi mbalimbali, tunaamini wawakilishi watatuwakilisha na kuhakikisha tunapata soko, stendi ili tupate maeneo mazuri ya kufanyia biashara zetu,” amesema.
Mgombea ubunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya ametaja mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati, hospitali ya halmashauri, vituo vya afya na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa nyumba za madaktari.
“Oktoba 29, 2025 tuna sababu ya kukuchagua kwa sababu katika sekta ya afya umeahidi ukishinda tena, ndani ya siku 100 utaboresha sekta hii. Umesema hutaki kuona mjamzito anayeenda hospitali kujifungua na kudaiwa vifaa vya kujifungua, wazee watapata matibabu bure.
“Elimu hujatuacha, madarasa zaidi ya 50, matundu vya vyoo zaidi ya 131 yamejengwa. Katika sekta ya maji zaidi ya Sh26 bilioni zimetengwa ili kukamilisha miradi tisa ya maji wanawake wa jimbo hili watuliwe ndoo kichwani na mradi huo unaendelea ambapo zaidi ya Sh13.7 bilioni zimetolewa,” amesema.
Mgombea huyo amesema mbali na mradi huo, pia wanatarajia kujenga tenki lenye ujazo wa lita milioni tano ili kusambaza maji kwenye kata za jimbo hilo.
Mgombea ubunge Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola ameeleza namna mgombea huyo ameboresha sekta mbalimbali jimbo kwake ikiwemo sekta ya elimu ambapo amefanikisha ujenzi wa madarasa 78 kwa shule za msingi na madarasa 68 ya sekondari.
“Kuna mengi umetutendea katika wilaya yetu, vituo vya afya vimeboreshwa na kujengwa, barabara pia umetuletea boti na umesaidia vijana wetu katika ufugaji wa samaki kwa kuwawezesha kuwa na vizimba,” amesema.

Amesisitiza kuwa Oktoba 29, 2025 wananchi wa Mwibara watajitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea huyo wa urais ili aendeleze aliyoyaanzisha.