Dar es Salaam. Wakati Kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiingia siku ya 43 leo Oktoba 9, 2025, mgombea urais wa Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru ameeleza tathimini ya chama Chake kwenye kampeni hizo.
Kunje ambaye kesho Oktoba 10, ataendelea na kampeni katika Mkoa wa Tabora kisha kuendelea mikoa ya kanda ya ziwa amesema, katika tathimini yake kwenye mikoa ya Kusini na ile ya Nyanda za Juu Kusini ambayo AAFP imefanya kampeni amebaini kero za wananchi ni zile zile.
Alizitaja kuwa ni kwenye afya akidai vituo vya afya vingi katika maeneo walikofanya kampeni navyo havina afya, vivyo hivyo kwenye elimu, miundombinu na hali ngumu ya maisha kwenye Kaya nyingi.
Katika tathamini yake, amesema nchi ya Tanzania ni tajiri na wananchi wake wanahitaji kuwa na maisha bora ambayo kama Watanzania watampa ridhaa ataboresha maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 9, 2025 katika mkutano uliofanyika makao makuu ya AAFP, Temeke jijini hapa, Kunje amesema akipewa ridhaa ya kuwa Rais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu Serikali yake itatoa bure bodaboda kwa kila kijana aliyevuka miaka asiye 18 ili imsaidie kuingiza kipato.
“Vilevile kwa kuwa Chama chetu ni Cha wakulima, kila kijana nitampa power tiller bure, kutakuwa na utaratibu mzuri wa kugawa hivi vitu kupitia Halmashauri ili vijana wakajiajiri na kuondokana na tatizo la ajira,” amesema.
Amesema pia atatoa trekta kwa kila Kaya 10, ili kuendeleza kilimo ambao ni uti wa mgongo kwa taifa huku akisisitiza mkakati wake wa kutokomeza mafisadi.
“Kwenye Serikali yangu, ukila pesa ya Umma nawe lazima uliwe na mamba,” amesisitiza Kunje akibainisha mkakati wake wa kujenga bwawa la mamba Ikulu endapo atapewa ridhaa kwa ajili ya kuwatumbukiza mafisadi.
Akizungumzia muendelezo na tathimini ya kampeni za chama hicho, Kunje amesema hadi sasa ana matumaini ya ushindi kwa asilimia 70 kutokana na muitikio wa wananchi kwenye mikoa aliyokwishafika kuomba ridhaa.
“Asilimia 30 iliyosalia, 20 ipo kwenye mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo ndipo tunaelekea kuanzia kesho (Oktoba 10), tutaanzia Tabora kisha tunakwenda kwenye mikoa yote ya kanda ya Ziwa ambako kuna tunaamini kuna asilimia 20 ya kura zetu huko,” amesema.
Aidha Kunje amegusia sintofahamu ya watu kupotea au kutekwa na watu wasiojulikana akibainisha kwamba, katika Serikali yake akipewa ridhaa hilo litakuwa historia.
“Lazima tujue mtaa una watu wangapi, Watanzania ni wa ngapi na wageni wanaoingia, hiyo ndiyo kazi ya Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa, haiwezekani mwenyekiti watu wanaingia mtaani kwako haujui,” amesema.