Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amewahamasisha watumishi wa umma kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza katika kikao cha tatu cha Baraza la Nane la Wafanyakazi kilichofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili, Mkomi alisema licha ya kutokuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, ana mapenzi na ustawi wa taifa, hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura, hasa watumishi wa umma, kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia.
“Nawaomba wenzangu watumishi wa umma tujitokeze kwa wingi siku ya Oktoba 29 kwenda kupiga kura huu ni wajibu wetu wa kikatiba na njia ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya nchi yetu,” alisema Mkomi.
Aidha, alibainisha kuwa hata viongozi wa kisiasa wamekuwa wakihamasisha familia zao kujitokeza kupiga kura, hivyo ni vyema pia kwa wafanyakazi wa umma kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kwa amani na utulivu.
“Niwaombe wajumbe wa baraza hili na watumishi wote, tusiwe nyuma. Tuwe mfano wa kuigwa katika kujenga demokrasia kwa kushiriki uchaguzi,” alisisitiza.
Kauli hiyo imekuja wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi ambao unatarajiwa kushirikisha wananchi katika kuchagua viongozi watakaowakilisha maeneo yao, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utawala bora na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya maendeleo.
Mwisho