Mradi wa Graphite, yametimia | Mwananchi

Dar es Salaam. Tanzania ipo katika hatua za mwisho kuanza kunufaika na madini yake ya Graphite, baada ya Serikali kwa kushirikiana na wawekezaji, kuanza utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini hayo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Madini Anthony Mavunde, mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300 (zaidi ya Sh740.37 bilioni), utaiweka nchi katika ramani ya dunia kama kitovu cha rasilimali muhimu ya teknolojia ya nishati safi.

Akizungumzia mradi huo leo, Alhamisi Oktoba 9, 2025, Mavunde amesema mradi huo wa Faru Graphite unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni ya Black Rock Mining (Australia).

Katika mradi huo, amesema Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa huku mwekezaji akimiliki asilimia 84, jambo linalohakikisha maslahi ya taifa yanalindwa bila kuzuia utaalamu wa sekta binafsi.

“Huu ni uwekezaji mkubwa unaoendana na dira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kinara kwa madini muhimu duniani,” amesema.

Amesema awali Tanzania ilichangia asilimia 0.6 tu ya usambazaji wa graphite duniani, ikiwa nyuma ya nchi za Msumbiji na Madagascar, lakini mradi huo utabadilisha takwimu hizo.

Katika maelezo yake, amesema graphite ni nyenzo muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme na uhifadhi wa nishati ya nyuklia.

“Kazi hii si mgodi tu, ni hatua ya mabadiliko ya viwanda,” amesema Waziri Mavunde, akisisitiza Faru Graphite imetoa nyumba mpya kwa wakazi waliopisha mradi kama sehemu ya uwajibikaji wa kijamii.

Ameeleza mradi huo utadumu kwa zaidi ya miaka 26 na utazalisha takribani ajira 900 za moja kwa moja na 4,000 zisizo za moja kwa moja.

Amesema utafungua fursa za mapato ya kaya na kuimarisha biashara ndogo na za kati katika huduma za malazi, chakula na usafiri.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Black Rock Mining, Paul Sims amesema zaidi ya ajira 400 tayari zitapatikana katika awamu ya kwanza na ndani ya awamu nne za ujenzi ajira za moja kwa moja zitafikia 900.

Amesema zaidi ya asilimia 75 ya vifaa vitatoka katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na zaidi ya asilimia 50 kutoka kwa wabia wa ndani, ili kuhakikisha manufaa yanabaki nchini.

Serikali imemteua Dk Teresa Yekwa kuwa Kamishna wa Mahusiano ya Ndani ili kusimamia utekelezaji wa sheria na ushiriki wa wazawa.

Mradi pia unafadhili ujenzi wa njia ya umeme ya kilomita 70 kutoka Ifakara hadi Mahenge, itakayounganisha mgodi na vijiji jirani na hivyo kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea viwanda vidogo.

Amesema mradi huo utatekelezwa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), itakayoboresha barabara na madaraja ikiwemo Faru-Jon Access Road, hatua itakayofungua uchumi na kuboresha usalama wa usafirishaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Faru, John de Vries, amesema ujenzi tayari umeanza na mgodi utazalisha tani 90,000 za graphite kwa mwaka katika awamu ya kwanza na baadaye utaongezwa kupitia moduli nne za uzalishaji.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema mapato ya kodi, leseni na michango ya kijamii kutoka mradi huo yataimarisha elimu, afya na miundombinu nchi nzima.