Mwili wa mgombea ubunge CUF aliyeuawa kuzikwa Oktoba 11 Kigoma

Siha. Mwili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, Daudi Ntuyehabi, unatarajiwa kusafirishwa kesho, Oktoba 10, 2025, kuelekea kijijini kwao Kumlungwe, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, kwa ajili ya taratibu za maziko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 9, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, Daudi Ntuyehabi alifariki dunia Oktoba 7, 2025, baada ya kushambuliwa na kundi la watu zaidi ya wanane.

Maigwa amesema kuwa watu hao walimshambulia wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja, wakati alipokuwa akijaribu kuingilia kati na kusuluhisha ugomvi uliomhusisha yeye na mtu mwingine waliokuwa wakizozana kuhusu deni kwenye ‘grocery’ ya vinywaji baridi.

Katika tukio hilo, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kujichukulia sheria mikononi, baada ya kumshambulia mgombea huyo wa ubunge na kumsababisha kifo.

Akizungumza na Mwananchi jioni ya leo, Oktoba 10, 2025 dada wa marehemu, Annet Ntuyehabi amesema kuwa mwili wa mdogo wake unatarajiwa kuchukuliwa kesho asubuhi kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kupelekwa Kijiji cha Kilingi, Sanya Juu, ambako alikuwa akiishi, ili kutoa fursa kwa ndugu, jamaa na marafiki kuuaga kuanzia saa nne asubuhi.

Amesema baada ya taratibu za kuaga zitakapomalizika,  wataanza safari jioni kuelekea mkoani Kigoma  ambapo ndugu yao huyo atazikwa kwenye makaburi ya familia siku ya Jumamosi Oktoba 11, 2025.

“Tutaaga kesho asubuhi kuanzia saa nne, ili kutoa fursa kwa  majirani, ndugu jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho kwa kaka yetu, na kisha tutaondoka  saa 11 jioni kwenda kijijini kwetu Kumlungwe ili kumpumzisha ndugu yetu kwenye nyumba yake ya milele,” amesema dada wa mgombea huyo.

Kwa upande Katibu wa CUF, Jimbo la Siha, Adam Ramadhan amesema chama hicho  pamoja na wadau wengine wanaendelea na taratibu mbalimbali za kuratibu safari ya kusafirisha mwili wa mgombea huyo kuelekea mkoani Kigoma.