WiLDAF TANZANIA NA GIZ WAENDESHA KAMBI MAALUM YA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUELEKEA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Mkurugenzi wa WiLDAF Tanzania, Anna Kulaya

Dar es Salaam, 09 Oktoba 2025

Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF Tanzania) kwa kushirikiana na GIZ, wameendesha Kambi Maalum ya Mafunzo kwa Waandishi wa Habari kwa muda wa siku tatu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka 2025, na kuunga mkono juhudi za kitaifa kupitia Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ukatili wa Kidijitali na Ukatili Dhidi ya Wanawake katika Uchaguzi.

Kupitia mafunzo haya, washiriki watajifunza namna bora ya kuripoti matukio yanayohusu ukatili wa kijinsia kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma, huku wakitumia teknolojia kwa usalama na kwa manufaa ya jamii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa WiLDAF Tanzania, Anna Kulaya alisema kuwa mpango huu ni sehemu ya jitihada endelevu za kujenga mtandao wa wanahabari wanaochochea mabadiliko ya kijamii kupitia uandishi unaolinda hadhi, haki na usawa wa kijinsia.

“Tunataka kuona waandishi wa habari wanakuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti za wanawake na wasichana, kupinga ukatili wa aina zote, na kutumia teknolojia kwa njia salama na chanya,” Wakili Anna Kulaya alisema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa GIZ alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya habari katika kupambana na ukatili unaochochewa na teknolojia, hasa ule unaowalenga wanawake katika siasa na uchaguzi.

“Kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika bila hofu ni msingi wa demokrasia. Kupitia mafunzo haya, tunajenga kizazi cha waandishi wa habari wanaotetea haki, usawa na uwajibikaji wa kijamii,” aliongeza.

Kambi hii pia ni sehemu ya maandalizi ya kuunga mkono Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ukatili Unaotokana na Teknolojia na Ukatili Dhidi ya Wanawake katika Uchaguzi, ambapo wadau kutoka serikali, asasi za kiraia, vyombo vya habari, na wadau wa maendeleo watakutana kujadili mikakati ya pamoja ya kukomesha ukatili wa kijinsia mtandaoni na nje ya mtandao.

WiLDAF Tanzania na GIZ wamesisitiza dhamira yao ya kuendelea kuwekeza katika elimu, uhamasishaji na ubunifu wa kimawasiliano ili kukuza jamii yenye usawa wa kijinsia na yenye heshima kwa haki za binadamu.