Dar es Salaam. Ingawa kamera za CCTV zimekuwa ngao muhimu ya ulinzi, usalama na ukusanyaji wa ushahidi, kwa upande mwingine, ufungaji wake, hasa nyumbani, unahitaji umakini ili kuepuka uvunjaji wa faragha na sheria.
Kwa mujibu wa wataalamu wa teknolojia na muktadha wa kisheria, ufungaji wa kamera hizo katika baadhi ya maeneo, mathalan chooni, bafuni, vyumba vya kubadilishia nguo na vyumba vya kulala ni kinyume na sheria, kwani maeneo hayo yanahusisha faragha za wahusika.
Watalaamu hao wamekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa, kufunga kamera za ulinzi katika maeneo hayo, kunakiuka haki ya faragha na usalama wa mtu, inayotakiwa kulindwa kwa mujibu wa sheria na matamko mbalimbali ya haki za binadamu ya kimataifa.
Suala la ufungaji wa kamera hizo, lina baraka za kisheria, yapo masharti ya maeneo zinakopaswa kufungwa, sio kila mahali, kwa mujibu wa Jimmy Makonde, ambaye ni mwanasheria.
Miongoni mwa masharti hayo, anasema ni kulindwa kwa faragha za watu, kama ilivyoabainishwa katika Ibara ya 16(1) ya Katiba ya Tanzania inayosema, “kila mtu anastahili heshima ya maisha yake binafsi na faragha yake.”
Masharti ya ufungaji wa kamera hizo hayakuishia kwenye Katiba ya nchi pekee, anasema hata kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kinabainisha hilo.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, ni marufuku kukusanya, kurekodi, au kusambaza taarifa za mtu bila ruhusa yake na kinaeleza adhabu yake ni faini hadi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.
Si hivyo tu, Makonde anasema hata Sheria ya Kanuni za Adhabu Kifungu cha 138B, kinazungumzia hilo, kikizuia kufuatilia au kumrekodi mtu akiwa kwenye mazingira ya faragha ni kosa la unyanyasaji wa kingono.
Lakini, ufungaji wa kamera hizo, anasema unahalalishwa na Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2017, inasema ushahidi lazima uwe halali kwa njia ya kisheria.
Hata hivyo, inasema ushahidi wa video iliyorekodiwa kwa uvunjaji wa faragha hupoteza uhalali, inaweza kutupiliwa mbali mahakamani na hata aliyeirekodi akafunguliwa kesi mpya.
Kifungu cha 4(d) cha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kinatoa msisitizo wa kuweka utaratibu wa kisheria na kitaasisi wa kulinda taarifa binafsi.
Sambamba na yote hayo, anaeleza kuwa Tanzania imeridhia mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) ambao kifungu 17, kinasema “hakuna mtu anayepaswa kuingiliwa faragha yake bila sababu.”
Akizungumza na Mwananchi kuhusu kamera hizo, Mtaalamu wa Masuala ya Teknolojia, Dominick Dismas amesema ufungaji wa kamera za CCTV ni muhimu kwani zinasaidia kubaini matukio ya kihalifu, hivyo kusaidia kuimarisha ulinzi katika eneo husika.
Dismas pia amesema picha ya CCTV zinavisaidia vyombo vya ulinzi na usalama kubaini mtendaji wa uhalifu kwa urahisi zaidi.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa ufungaji wake unapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya kijamii na kulinda haki ya faragha.
“Ndiyo maana maeneo kama vyoo, bafu, vyumba vya kubadilishia nguo na vyumba vya hotelini hayaruhusiwi kufungwa kamera za CCTV ili kulinda faragha,” amesema.
Amesema kamera za aina hiyo zinashauriwa kufungwa katika maeneo ya biashara, nje ya nyumba, hospitali, ofisini na maeneo mengine ya umma.
“Hata katika ofisi ni kosa kufunga kamera hizo katika ofisi ya mtu mmoja mmoja na hata hospitalini hairuhusiwi kufunga ndani ya vyumba vya wagonjwa,” amesema.
Anaongeza kuwa hata inapotokea mtu amefunga kamera hizo mahala sahihi na ikatokea amebaini kufanyika kwa kitendo cha kihalifu, anashauriwa kuripoti katika mamlaka husika na si kusambaza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika mitandao ya kijamii.
Akichangia mada hiyo, Msimamizi masuala ya Usalama wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Apoo Justus amesema kamera zinazofungwa katika taasisi au maeneo ya biashara, inashauriwa kuambatana na mabango yanayoonyesha kwamba eneo hilo linachunguzwa.
“Kuna umuhimu wa kuwajulisha watu kwamba eneo fulani lina CCTV, inasaidia kulinda haki ya faragha,” amesema.
Anaeleza kuwa changamoto zinazojitokeza zinasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ugeni wa teknolojia hiyo, kwani imeanza kutumika sana miaka ya hivi karibuni.
Pia, ufungaji wa vifaa hivyo ambavyo ni muhimu kwa masuala ya usalama kufanywa na watu wasio na utaalamu kwa kigezo cha uzoefu.
“Baadhi ya watu wanafanya kazi ya kufunga kamera kwa sababu wamejifunza tu kufanya hivyo, hawajui sheria wala miiko yake, hili nalo linachangia,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa ni muhimu elimu kuendelea kutolewa kwa wanaofanya shughuli hizo na hata wananchi kwa ujumla, ili kusaidia kulinda haki ya faragha.
Amesisitiza ukiacha faida za kuimarika kwa ulinzi, usalama na kukusanya ushahidi, ufungaji wa kamera hizo hasa nyumbani, unahatarisha haki ya faragha na kukinzana na matakwa ya sheria.
Rehema Kihwele, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema katika juhudi za kuhakikisha usalama wa mtoto wake anapokuwa mbali naye, alitaka kufunga kamera za CCTV katika chumba anachoishi mtoto huyo pamoja na msaidizi wa kazi za nyumbani.
Hata hivyo, mtaalamu aliyemwajiri kwa ajili ya kufunga kamera hizo, alikataa kufanya hivyo, akieleza kuwa jambo hilo haliruhusiwi kisheria.
“Kiukweli kwa wakati ule sikuwa na uelewa kuwa kufanya hivyo ni kosa, nilitaka tu kufanya hivyo ili kumlinda mtoto wangu, kumbe ningekuwa navunja sheria,” amesema.
Abdallah Komba, mmiliki wa duka eneo a Kariakoo, amesema kamera zimemsaidia kufuatilia wafanyakazi wake na kudhibiti wizi, lakini anasisitiza matumizi yake ni yenye mipaka.
“Zinasaidia sana katika biashara, lakini lazima zitumike kwa heshima, si vizuri kuzitumia kurekodi mambo binafsi ya watu,” alisema.
Ali Athumani anatoa wito kwa watu waliofunga kamera hizo kuacha kusambaza hovyo video zilizorekodiwa kupitia vifaa hivyo na pale inapotokea masuala ya kihalifu au uvunjwaji wa sheria ni vyema kuripoti katika mamlaka husika.