Vyeti vya mabaharia wa Tanzania mbio kutambulika Ulaya

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mohamed Salum amesema Tanzania ipo hatua za mwisho kuhakikisha vyeti vya mabaharia vinavyotolewa nchini vinatambulika na Umoja wa Ulaya (EU).

Amesema kutambulika kwa vyeti hivyo kutafungua fursa nyingi za ajira kwa mabaharia wa Tanzania.

Salum ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani’ hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Kukubalika kwa vyeti vyetu na EU kutamaanisha mabaharia wa Tanzania wataajiriwa kwenye meli za Ulaya bila vikwazo vya kisheria. Hii ni hatua kubwa katika kukuza ajira na uchumi wa baharini,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine Salum amesema shirika hilo limeanza mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuboresha huduma kwa mabaharia na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri majini, kupitia mpango wa utoaji wa vyeti vya kidijiti kwa mabaharia.

“Kupitia mfumo huu, mabaharia  watapata na kuthibitisha vyeti vyao kwa urahisi zaidi, popote walipo duniani, vyeti vitakuwa na alama za usalama za kimataifa kama QR Code na sahihi za kielektroniki ili kuondoa uwezekano wa kughushi,” amesema  Salum.

Kwa upande mwingine, Salum ameitumia hafla hiyo kuhimiza wafanyakazi wa TASAC kujituma na kushirikiana.

Amesisitiza huduma bora kwa mteja si maneno tu bali ni matendo hivyo mageuzi ya kidijitali ndiyo uthibitisho wa huduma bora.

Aidha Salum amesema TASAC inaendelea kuboresha mifumo yake ya kidijitali,  kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kitovu cha huduma bora za usafiri majini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.

Mfumo huo, ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya kuimarisha huduma kwa wateja kwa kutumia Tehama na kujenga uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma.

Hamis Juma mmoja wa mabaharia waliohudhuria katika maadhimisho hayo amesema kuanza kwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki kutawapunguzia gharama na muda wanaotumia kupata au kubadilisha vyeti.

“Hapo zamani ilikuwa lazima usafiri hadi ofisi za TASAC, lakini sasa tunaweza kuthibitisha vyeti kwa njia ya mtandao, hii ni hatua ya kihistoria,” amesema.