WAKILI aliendelea: “Wakati mwingine makosa ya watendaji wa serikali yanaweza kusababisha makosa mengine kwa wananchi. Mshitakiwa bado ni kijana mdogo sana. Alipoona watu waliomuua ndugu yake wametoroshwa jela, alitokwa na imani na watendaji wa serikali. Alishindwa hata kwenda kupiga ripoti polisi, na kutokana na imani kwamba wale watu walishahukumiwa kunyongwa, akaona afanye yeye kazi hiyo.”
Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi alisema:
“Ninaiomba mahakama yako imuachie huru mshitakiwa kwa kumuona hana hatia. Na kama itamuona ana kosa, impe adhabu ndogo.”
Baada ya kumaliza maelezo yake, wakili wa utetezi akavuta kiti na kukaa.
Jaji aliandika maelezo yake, kisha akamtazama wakili huyo.
“Kwa vile mshitakiwa ameamua kukiri kosa yeye mwenyewe, haitajiki kuita mashahidi. Tuliita mashahidi wa upande wa mashitaka kwa ajili ya kutaka kujiridhisha kama kweli mshitakiwa ametenda kosa alilokiri,” Jaji alimwambia wakili huyo.
Akaendelea: “Kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhika kwamba mshitakiwa ametenda kosa aliloshitakiwa nalo, na ambalo yeye mwenyewe amelikiri.”
“Katika maelezo yako ya mwisho, wakili wa utetezi, umemtetea mshitakiwa kwamba hastahili kupatikana na hatia kwa sababu shitaka lake ni batili, kwa kile ulichodai kwamba mshitakiwa hakustahili kushitakiwa kwa kosa la mauaji, bali alistahili kushitakiwa kwa kosa la kujitwalia mamlaka ya kunyonga watu waliohukumiwa kunyongwa wakati haikuwa kazi yake,” jaji aliendelea kueleza.
Akahitimisha maelezo yake kwa kusema kuwa amepokea maelezo kutoka pande zote mbili — upande wa mashitaka na upande wa utetezi — na kwamba angetoa hukumu ya kesi hiyo baada ya mwezi mmoja.
Baada ya hapo, kesi iliahirishwa. Mimi, afisa upelelezi pamoja na wakili wa serikali tuliingia katika ofisi ya mawakili na kujadiliana juu ya hukumu ya kesi ile.
Wakili wa serikali akatuambia kwamba hakuwa na shaka yoyote kuwa Faustin atapatikana na hatia na adhabu yake itakuwa kifo.
“Naona wakili wake amechachamaa sana kutaka kuibadili hii kesi,” nikasema.
“Tangu mwanzo wa kesi alionekana kutaka lile shitaka libadilishwe, lakini isingewezekana kwa sababu mshitakiwa ameua na ameshitakiwa kwa kosa la kuua,” alisema afisa upelelezi.
“Kama wakili wa utetezi, ni lazima atafute hoja yoyote tu, hata kama iko nje ya sheria, ilimradi aonekane amefanya kazi yake. Lakini tunaamini kuwa mahakama itatoa haki kwa mujibu wa sheria,” alisema tena afisa upelelezi.
“Sasa yeye alitaka shitaka liwe la kujitwalia mamlaka. Lengo lake ni kumuepusha mshitakiwa na adhabu ya kifo, jambo ambalo haliwezekani kwa sababu mshitakiwa ameua kinyume cha sheria,” wakili wa serikali aliendelea kufafanua.
Baada ya kumaliza mjadala wetu, mimi na afisa upelelezi tuliondoka mahakamani. Afisa upelelezi alikwenda ofisini kwake, na mimi nikaenda ofisini kwangu.
Katika kipindi hicho maandalizi ya harusi yangu na Hamisa yalikuwa yakiendelea. Tulikuwa tumebakisha majuma machache tu tufunge ndoa.
Nilishakutana na wazazi wa Hamisa mara kadhaa na kulizungumzia suala hilo na kukubaliana. Pia nilishatoa taarifa kwa wakuu wangu wa kazi kwamba nilikuwa najiandaa kuchukua jiko katika siku ambayo ningewatangazia.
Nilikuwa nimeanzisha kawaida ya kwenda nyumbani kwa Hamisa karibu kila siku. Siku ambayo sikwenda kwa Hamisa nilipaswa nimpe sababu kwa nini sikufika nyumbani kwake.
Kwa kutaka kumuandaa kwa ajili ya chakula cha usiku ambacho mara nyingi tunakula hotelini, nilimpigia simu na kumjulisha asipike kitu.
“Tutakwenda kula wapi chakula cha usiku?” akaniuliza.
“Tutakwenda kula Nyumbani Hotel.”
“Sawa, sitapika. Utakuja saa ngapi?”
“Saa moja usiku.”
“Nitakusubiri.”
Dakika chache kabla ya saa moja usiku, nilibisha mlango wa nyumba ya Hamisa.
“Karibu!” sauti ya Hamisa ilisikika kutoka ndani.
Baada ya sekunde chache, mlango ukafunguliwa.
“Karibu ndani,” Hamisa akanikaribisha.
Sikukaribishwa na sauti ya Hamisa pekee, nilikaribishwa pia na kupuliziwa harufu ya manukato yaliyotoka mwilini mwake, ambaye tayari alikuwa amevaa nguo za kutokea.
Hamisa alinipisha mlangoni, nikaingia ndani kisha akaufunga mlango.
Nilikwenda kukaa kwenye kochi nikamtazama Hamisa. Televisheni yake ilikuwa imewashwa; msanii maarufu alikuwa akiimba wimbo wa mapenzi.
Katika wimbo huo, msanii huyo alikuwa akisisitiza kuwa ameshakamilisha maandalizi ya ndoa yake na yule ampendaye, hivyo baada ya siku chache tu watakuwa bwana na bibi harusi.

Hamisa alipoondoka mlangoni, alikuwa akiimba wimbo huo huku akitabasamu na kutikisika.
Alikuja kuketi kando yangu na kuniimbia wimbo huo sikioni kwangu. Alikuwa kama ananinong’oneza kitu.
Nikafahamu maana ya kuniimbia wimbo huo — siku za ndoa yetu zilikuwa zimekaribia sana.
“Nimeweka wimbo huo kwa ajili yako,” akaniambia baada ya kuniimbia mistari miwili ya wimbo.
“Najisikia sana,” nikasema.
“Kwanini?”
“Mistari uliyonipa imenipa msisimko na kunikumbusha mengi.”
“Kama yapi?”
Sikushangaa Hamisa aliponiuliza swali ambalo jibu lake alikuwa analijua. Mara nyingi ndivyo wapenzi wawili wanavyokuwa wanapozungumza.
“Kuhusu ndoa yetu. Najiona nina wajibu wa kuzingatia kwamba ndoa ni pingu za maisha,” nikamwambia.
“Kwako na kwangu?”
“Ndiyo.”
“Na ndiyo mustakbali wetu utakavyokuwa?”
“Ndiyo.”
“Hakuna shaka kwamba mioyo yetu inasubiri kwa hamu kuiona siku hiyo inawadia.”
“Ndiyo.”
Hamisa akacheka. Nilijua kilichomchekesha ni kulirudia kwangu kwa mkazo tamshi hilo la ‘ndiyo’ mara nyingi.
Kwa vile kukaa kwake karibu nami kulinisisimua, nikamshika shavuni kisha nikamuuliza: “Umeshajiandaa kutoka?”
“Mimi niko tayari, nilikuwa nakusubiri wewe tu.”
“Basi tunaweza kwenda.”
Hamisa akatangulia kuinuka. Alikuja mbele yangu, akaishika mikono yangu na kuniambia:
“Ngoja nikuinue.”
Baada ya kuishika mikono yangu, alinivuta kuniinua. Nikainuka.
“Ngoja nizime TV, twende.”
Alizima televisheni, akaingia chumbani kwake kuchukua mkoba wake. Alipotoka, tuliondoka.
Nilimrudisha Hamisa nyumbani kwake saa sita usiku. Alipoingia ndani, mimi nikaondoka.
Asubuhi ya siku iliyofuata, majira ya saa tatu, mama yake Faustin aliwasili ofisini kwangu.
Baada ya kunisalimia, aliniambia: “Nimekuja kukuaga, leo ninaondoka kurudi Lindi.”
Tulikuwa naye wakati wote wa kesi ya Faustin. Siku ambazo kesi ilikuwa inaahirishwa, alikuwa akirudi Lindi na kukaa hadi kesi inapoitishwa tena ndipo anakuja.
“Unaondoka leo?” nikamuuliza: “Ninaondoka leo. Nitarudi kabla ya hukumu ya mwanangu kutolewa.”
“Sawa, uende salama.”
Akanyamaza kimya kwa sekunde kadhaa, kisha akaniambia: “Nitakuja tena niagane na mwanangu. Najua baada ya hukumu sitaonana naye tena.”
“Baada ya hukumu kesi itakuwa imemalizika.”
“Ndiyo maana nikasema sitaonana naye tena, kwa sababu najua kuwa atanyongwa.”