Dar es Salaam. Kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kumeendelea kuzua mjadala mpana, baada ya wabunge wa Umoja wa Ulaya (EU) kulaani tukio hilo na kulitaja kuwa la kutisha linalohitaji hatua za haraka.
Katika taarifa iliyotolewa jana Oktoba 10, 2025, kwa pamoja na wabunge wa EU, Barry Andrews, Robert Biedrón, Udo Bullmann, Michael Gahler, Erik Marquardt na David McAllister, wamesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu matukio ya utekaji na ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa kisiasa, wakosoaji wa Serikali na waandishi wa habari nchini Tanzania.
“Tunatoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha usalama wa Polepole na kuchukua hatua madhubuti kumaliza mwenendo wa vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) pia kulaani tukio hilo na kuitaka Serikali kuchunguza kwa kina hali ya kutoweka kwa Polepole.
Polepole, ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, alitekwa usiku wa kuamkia Oktoba 6, 2025, katika makazi yake yaliyopo Ununio, Dar es Salaam.
Tayari Jeshi la Polisi, kupitia Msemaji wake David Misime, limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini ukweli wa kilichotokea.
Endelea kufuatilia Mwananchi