SERIKALI YATOA SHILINGI TRILIONI 3.5 KUWEZESHA VIJANA KIUCHUMI -MAJALIWA

Na. OWM (KVAU) – MBEYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi trilioni 3.5 kufikia mwaka 2024 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kutoka shilingi bilioni 904 mwaka 2021.

Amesema fedha hizo zimewasaidia vijana kupata mitaji ambayo imewawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hatimaye kuinua vipato vyao pamoja na uchumi wa Taifa.

Amesema hayo leo Ijumaa (Oktoba 10, 2025) wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa iliyofanyika mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ni Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imefanya hivyo kwa kutambua kuwa Vijana ni nguvu kazi na ndiyo msingi wa safari ya maendeleo ya Taifa. “Vijana wakipewa nafasi na kuandaliwa ipasavyo, wanaweza kuwa nguzo kuu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kufanikishaMalengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs)”.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza Vijana wamekuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na wamechangia kwa kiwango kikubwa katika kilimo, biashara, teknolojia, michezo na sanaa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema, Serikali inatambua umuhimu wa kundi la Vijana na ndiyo maana inawekeza na kuthamini mchango na nguvu zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“Hii ni rasilimali kubwa ambayo ikielekezwa na ikijengewa uwezo ipasavyo kupitia vipaji walivyonavyo italeta maendeleo endelevu na kujenga Taifa shindani na lenye ustawi”.