Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Maswa
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema mkakati wa Serikali ni kujenga skimu za umwagiliaji 738 nchini kote lengo likiwa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumza leo Oktoba 11,2025 akiwa wilayani Maswa akielea mkoani Shinyanga akiendelea na mikutano ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo itajenga skimu za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Dk Samia amesema katika sekta ya kilimo walianza na mfumo wa kutoa ruzuku katika pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ya ruzuku,kutoa ruzuku ya chanjo kwa mifugo, kwa sasa pia mkakati ni kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na kwamba zitajengwa skimu 738 nchi nzima na mkoani Shinyanga nako zitajengwa.
Amesema lengo lake ni kuona sekta ya kilimo inakuwa kwa asilimia 10 kutoka asilimia tano ya sasa.”Nataka wakati naenda Kizimkazi kupumzika niiache sekta ya kilimo imekuwa kwa asilimia. Ninapozungumzia kilimo namzungumzia pia mifugo na uvuvi.”
Wakati akianza kuzungumza na wananchi hao waliojitokeza kwa wingi mapema asubuhi mgombea Urais Dk.Samia amewashukuru kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo na hiyo inaonesha mapenzi yao kwa Chama hicho na katika Uchaguzi mkuu CCM inakwenda kushinda.
“Leo nauaga Mkoa wa Simiyu hapa Maswa wakati naingia Mkoa huu niliingilia Lamadi .Kwa hapa Maswa na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla tumefanya maendeleo katika sekta mbalimbali.Tunapozungumza mafanikio miaka mitano nawapongeza Maswa.
“Yaliyofanyika Maswa yamefanyika pia Tanzania yenye mikoa 26 na Zanzibar mitano,kazi ni hii ya kuleta maendeleo ni kwa kila Wilaya na kila Mkoa .”
Dk.Samia amesema kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo hayo ni wazi CCM inaonesha uwezo wa kuwatumikia Watanzania.
“Moja ya kauli yangu niliyowahi kuitoa ni nitafanya maendeleo na Serikali yangu na wananchi watasema,kuna mengi yaliyofanyika,Tumefanya na tutaweza kufanya.
“Niwapongeze Maswa kwa mambo makubwa yaliyofanyika katika sekta mbalimbali.
Na tunakwenda kuendelea na kazi kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma,anapata maji safi na salama.
Anapata umeme,huduma za afya karibu, miundombinu ya barabara.Katika elimu kila mtoto awe na fursa ya kupata elimu.