Wakulima, wavuvi waahidiwa vifaa vya kisasa CCM ikirejea madarakani

Unguja. Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi ameahidi neema kwa wavuvi, wakulima wa mwani na mpunga kwa kutoa zana za kisasa kuongeza uzalishaji.

Ametoa ahadi hizo leo Oktoba 11, 2025 wakati akizungumza na makundi ya  wakulima wa mwani, mpunga na wavuvi katika Shehia za Marumbi na Cheju Jimbo la Chwaka Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za chama hicho

Kuhusu kilimo cha mpunga, Dk Mwinyi amesema pamoja na kuendeleza kilimo cha kisasa, watatoa mbolea, mbegu  na viuatilifu kuongeza uzalishaji wenye tija.

“Licha ya Zanzibar chakula chetu kikuu kuwa wali, lakini bado uzalishaji wa mpunga ni kidogo na tunaagiza kutoka nje ya nchi, ni kweli hatuwezi kuzalisha cha kutosheleza kabisa lakini tunawajibu wa kupata chakula cha kutosha,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema baada ya kuwawezesha wakulima na kuzalisha mpunga kwa chakula na biashara, Serikali itakuwa ikinunua mpunga huo hivyo wasiwe na shaka na upatikanaji wa soko.

Mkulima wa mpunga Haji Salum amesema katika bonde la Cheju kuna hekta 680 ambazo zinatumiwa na wakulima 6000 baada ya kuwekewa miundombinu ya kisasa.

Hata hivyo amesema bado uzalishaji ni kidogo na ardhi sehemu nyingi inaharibika.

Akizungumza kwa sekta ya ukulima wa mwani, mgombea huyo amesema Zanzibar ndio mzalishaji mkubwa wa mwani Afrika, hivyo wana kila sababu ya kutoa kipaumbele na mkazo wa kuhakikisha zao hilo linaendelea kuongezeka.

“Hapa imezungumzwa kuhusu bei, tutatoa bei nzuri ya Sh1000 na tutanunua sisi na kujenga viwanda vya mwani,” amesema

Amesema watatafuta utaratibu mzuri ili kusiwe na mwingiliano wa kilimo cha mwani, uvuvi na utalii li kila sekta inaendelea kuleta tija kutokana na umuhimu wake.

Kwa upande wa uvuvi Dk Mwinyi amesema wataendelea kutoa vifaa vya kisasa ili wavuvi wakavue maji ya kina kirefu.

“Tunahitaji boti kubwa na zana za kisasa na nyavu za uvuvi zinazokubalika kisheria,” amesema Dk Mwinyi

Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya wakulima wa mwani, Fatma Abdulla ameomba kuangaliwa na kushughulikiwa changamoto zao akitaja bei kuwa bado ni tatizo.

“Vifaa vya mwani vimesombwa na maji, bei za mwani Bado ina changamoto haisimami, tunaomba tuangaliwe na kupatiwa elimu ya ukulima,” amesema

Pia amelalamikia nyavu zao kuvurugwa na baadhi ya wavuvi hivyo kupata hasara.

Naye Foum Ali Foum akizungumza kwa niaba ya wavuvi amesema wao ni wadau wa uhifadhi wa bahari lakini hawanufaiki

Naye Rashid Amour amesema viongozi wengi katika sekta ya uvuvi wanatumia uamuzi wao wenyewe badala ya kutumia sheria zilizopo.

“Watendaji katika sekta hii wengi wanatumia akili zao na sheria zinawekwa pembeni hivyo inaibua changamoto kubwa,” amesema

Mvuvi mwingine Ali Omari ameomba sekta ya bahari irasimishwe na bado kuna uvuvi wa mazoea na kiwango kikubwa cha bahari bado hakijafikiwa.

Ameomba kuangaliwa sheria ya uvuvi ambayo haiendani na mazingira ya sasa kwani inazuia kuingia na vioo na kutumia viatu vya kuogelea mambo ambayo yanawatesa wavuvi.