Samia aahidi kuongeza udhibiti wanyamapori Kanda ya Ziwa

Maswa. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuongeza vituo zaidi vya ufuatiliaji kwa kutumia ndege nyuki  ‘drones’ katika wilaya ya Maswa na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa, ili kusaidia kudhibiti wanyama wakali  wanaovamia mashamba, kudhuru wananchi na kuimarisha doria.

Mgombea huyo ametoa ahadi hiyo leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 wilayani Maswa mkoani Simiyu katika mkutano wa kampeni kabla ya kuwasili mkoani Shinyanga anapoanza kampeni zake leo.

Amesema Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na tatizo la wanyama wakali wanaovamia vijiji vilivyoko karibu na hifadhi za wanyamapori.

 “Nataka niwape neno la faraja. Tumeanza kuchukua hatua na jana tu, kituo kimoja hapa Maswa kimekabidhiwa vifaa, vikiwemo drones zinazoweza kuona wanyama wakitoka mbugani na kwenda kuwarudisha,” amesema

 “Tutajenga vituo zaidi kama hivyo katika mkoa huu na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha wananchi na mashamba yao yako salama.”

Samia, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema serikali yake imepiga hatua kubwa katika kuboresha sekta muhimu kama elimu, maji, afya, umeme, kilimo na mifugo.

Amesema serikali itaendelea kutekeleza miradi ambayo haijakamilika na kuanzisha mingine mipya ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za kijamii.

“Nawapongeza kwa mafanikio tuliyoyapata katika sekta ya elimu, maji, afya na umeme. Lakini nataka niwaambie, hatujamaliza kazi. Tunaendelea kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya afya karibu, na kila mtu anapata maji safi na salama. Ndiyo maana miradi mingi ambayo haijakamilika inaendelezwa, na mingine mipya inaendelea kuanzishwa,” amesema.

Amesema serikali imejipanga kuhakikisha kila kitongoji nchini kinaunganishwa na umeme, akibainisha kuwa umeme ni nguzo muhimu ya maendeleo na usalama.

“Umeme ni maendeleo, ni usalama, na unaleta mwanga majumbani. Kama vile tunavyomuomba Mwenyezi Mungu atupe nuru, katika dunia hii nuru yetu ni umeme. Tumeunganisha vijiji vyote na sasa tunahamia kwenye vitongoji. Tunataka kila kaya iwe na umeme,” amesema.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Samia amezema serikali imeendelea kuwaunga mkono wakulima kupitia ruzuku za pembejeo, mbolea, miradi ya umwagiliaji, na chanjo kwa mifugo.

“Tumeanza vizuri na ruzuku za pembejeo na mbolea. Tumekarabati na kujenga minada mipya, na umwagiliaji ndiyo kipaumbele chetu. Ifikapo mwaka 2030, ninapotaka kustaafu kijijini kwetu, nataka niache sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 kwa mwaka, kutoka asilimia 4 au 5 tulizo nazo sasa,” alieleza.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuhimiza uanzishaji wa viwanda vitakavyosindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, ili kutoa ajira kwa vijana wanaohitimu katika vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi.

“Tunataka vijana wetu wapate ajira kupitia viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi,” ameema.

Samia alitaja miradi mikubwa ya miundombinu itakayochochea uchumi wa Simiyu, ikiwemo barabara ya bypass ya Sh18 bilioni na mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Arusha ambao utapita Maswa.

“Reli ya SGR itakuwa na kituo kikubwa hapa Maswa kwa ajili ya abiria na mizigo. Hii itakuwa fursa ya kibiashara kwa wananchi wetu,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohamed, aliishukuru serikali kwa mageuzi makubwa katika sekta ya pamba na hatua za kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakulima.

“Hapo awali wakulima wa pamba walikabiliwa na changamoto nyingi, lakini sasa serikali imetupa mbolea na viuatilifu. Kupitia Wizara ya Kilimo tumepata mwekezaji ambaye atajenga kiwanda Itilima. Kwa kuwa Simiyu ndio kinara wa uzalishaji wa pamba nchini, ushindani huu utasaidia bei kwa mkulima kupanda,” alisema Shamsa.

Aidha, alikiri kuwepo kwa changamoto ya wanyama wakali katika vijiji vilivyo karibu na hifadhi, lakini alionyesha matumaini kwamba serikali itaimaliza changamoto hiyo kupitia mpango wa utekelezaji wa 2025–2030.

“Vijiji vingi viko karibu na hifadhi, jambo lililosababisha changamoto ya wanyama wakali. Lakini kwa jitihada za serikali, ikiwemo ujenzi wa vituo vya drones, naamini tatizo hili litaisha katika miaka ijayo,” alisema.

Samia amehitimisha hotuba yake kwa kuonesha matumaini kwamba wananchi wataendelea kuiamini CCM kutokana na rekodi yake ya utekelezaji.

“Nilipoapa kuongoza nchi hii nilisema nitafanya kazi na wananchi wenyewe waseme,” amesema. CCM tumefanya, na tutaendelea kufanya. Tunaamini tuna uwezo wa kufanya zaidi kwa ajili ya Watanzania,” amesema