Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Elimu, Afrika Mashariki wakishirikiana na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), wamefanya matembezi yaliyohusisha kuhamasisha afya ya akili na ushirikiano kwa walimu na kufanya usafi wa mazingira.
Miongoni mwa taasisi zilizopo ndani ya AKDN ni zilizoshiriki matambezi hayo ni pamoja na Benki ya Daimond, Serena Hoteli, Hospitali ya Aga Khan, Aga Khan Foundation (AKF), Aga Khan Education Services na shirika la bima la Daimond Jubilee.
Usafi huo umefanyika ufukwe wa Bahari ya Hindi, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usafi wa mazingira.
Matembezi yamefanyika leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 yaliyoandaliwa na Chuu Kikuu cha Aga Khan, Taasisi ya Maendeleo ya Elimu, Afrika Mashariki, yaliyohusisha umbali wa kilomita tano yalianzia Daimond Jubilee, kwa kupita maeneo mbalimbali ya Upanga na kuishia fukwe ya Aga Khan Hospitali.
Mkuu wa AKU Tanzania, Profesa Eunice Pallangyo amewaambia wanahabari kuwa pamoja na wafanyakazi hao kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao pia wamejuika na Watanzania wengine kufanya usafi kwenye ufukwe huo ili kulinda mazingira ya rasilimali hiyo.
“Tunatambua umuhimu wa mazingira ndio maana, pia tumefanya usafi kutoka sehemu hadi nyingine. Leo tumefanya vitu vingi vya tofauti, lakini matembezi haya ni sehemu ya kusheherekea siku ya walimu, kama ambavyo inajulikana kila ifikapo Oktoba,” amesema.
“Walimu ni watu wa muhimu sana, ingawa mara kadhaa wanasahaulika, lakini hakuna hata mmoja asiyepita mikononi mwa walimu kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu. Lazima tusimame na kutambua thamani ya walimu,” amesema.
Profesa Pallangyo amesisitiza kuwa matembezi hayo yamelenga pia kumjengea Mwalimu umahiri na afya katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, wafanyakazi hao kwa umoja hao wameamua kujichangisha fedha za taslimu (hakuweka wazi kiasi) na kuzipeleka katika shule ya msingi ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, ili kuboresha baadhi ya miundombinu ya shule hiyo.
“Pia, tutatoa vitabu zaidi ya 1,000 kwa ajili ya kuhamasisha wanafunzi kujifunza na kujisomea kwa wanafunzi wa shule ya Muhimbili. Huu ni mwanzo tu kwa siku zijazo tupata kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road,” amesema Profesa Pallangyo.
Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya msingi Muhimbili, Boniface Mbena ameshukuru ushirikiano wa AKU, akisema taasisi hiyo ni majirani ya shule hiyo na mara kwa wamekuwa karibu katika shughuli za maendeleo.
“Kila mara AKU wamekuwa wakitusaidia na kutuwezesha vitu tofauti tofauti kwa wanafunzi, lakini pia kitaaluma.Msaada wa vitabu tutakaopewa utatusaidia katika kuimarisha usomaji na ujifunzaji, lakini utatouongezea pale tulipopungukiwa,” ameeleza Mbena.