Bashungwa: CCM ni dhamana ya amani, maendeleo

Karagwe. Mgombea ubunge wa Jimbo la Karagwe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Innocent Bashungwa amesisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuendelea kuongoza nchi kwa utulivu na amani.

Akihutubia wa kampeni uliofanyika jana Oktoba 10, 2025 katika Kijiji cha Nyakayanja, Kata ya Nyaishozi, Bashungwa amesisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuendelea kuongoza nchi kwa utulivu na amani, bila kuiingiza Tanzania kwenye machafuko au migogoro ya kisiasa.

“Katika kipindi cha miaka mingi, CCM imekuwa ikiongoza kwa misingi ya amani, umoja na maendeleo. Hakuna chama kingine kinachoweza kuhakikisha utulivu wa nchi kama CCM.

“Tuna sera zinazotekelezeka, tuna uzoefu wa kuongoza, na tuna viongozi makini waliowekwa na wananchi wenyewe,” amesema Bashungwa.

Pia, aliwataka wananchi wa Karagwe kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kwa kuchagua wagombea wa CCM katika ngazi zote za urais, ubunge na udiwani.

Bashungwa amesisitiza akisisitiza kuwa kura zao ni msingi wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Akizungumzia mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, Bashungwa alieleza kuwa ni wakati wa wanawake kuonyesha mshikamano wao kwa kumpigia kura za ndiyo.

“Zamu hii akina mama ni zamu yenu. Huyu ni mama mwenzenu, amepigana kwa bidii na sasa anastahili kuendelea kuiongoza nchi yetu. Naomba mpende, mshirikiane naye, na kura zote za akina mama ziwe kwake. Hii ni fursa ya kihistoria,” amesisitiza Bashungwa.

Aidha, alitumia mkutano huo kuomba ridhaa ya wananchi wa Karagwe kumchagua tena kuwa mbunge, akiahidi kuendeleza jitihada za kuboresha maisha ya wananchi kwa kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, na miundombinu ya barabara zinazounganisha vijiji na kata mbalimbali katika jimbo hilo.

Pamoja na hayo, alimuombea kura mgombea udiwani wa CCM katika Kata ya Nyaishozi, Wallace Mashanda, akimtaja kuwa ni kiongozi mchapa kazi ambaye ataweza kushirikiana na serikali na wabunge kuharakisha maendeleo ya kata hiyo.