Ushirikiano huo umeendelea kuzaa matunda kupitia miradi 48 ya ujenzi, ukarabati na umaliziaji wa miundombinu ya elimu inayotekelezwa na TEA kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), kwa ufadhili wa Serikali ya Canada katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo na kuweka vibao vya ufadhili, Afisa Miradi kutoka TEA, Bi. Atugonza David, alisema amefarijika kuona miradi yote ikiwa katika hatua nzuri na tayari kwa matumizi. Alibainisha kuwa asilimia kubwa ya miradi hiyo imejikita katika umaliziaji na ukarabati wa maabara za sayansi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza hamasa ya wanafunzi kupenda na kujifunza masomo ya sayansi.
Moja ya shule zilizonufaika na miradi hiyo ni Shule ya Sekondari Nyakitonto iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ambayo ilipokea takribani shilingi milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa maabara tatu za sayansi.
Akizungumza kwa niaba ya shule, Mwalimu Maisha Masabile, Makamu Mkuu wa shule hiyo, alisema mradi huo umeleta mabadiliko makubwa katika ufaulu wa wanafunzi.
“Awali hatukuwa na maabara hata moja, tulikuwa tukifanyia mazoezi ya sayansi darasani. Kupitia mradi huu, tumeweza kukarabati vyumba vitatu vya maabara na matokeo yake yamekuwa chanya. Mwaka 2024 ufaulu ulikuwa asilimia 100, huku wanafunzi 43 kati ya 150 wakisajiliwa kusoma masomo ya sayansi. Mwaka huu 2025, idadi imeongezeka hadi wanafunzi 68 kati ya 210, na wanaendelea kufanya vizuri,” alisema Mwalimu Masabile.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na UNICEF inaendelea kutekeleza miradi yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.5 katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe. Miradi hiyo inalenga kuinua ubora wa elimu, kupanua wigo wa fursa za kujifunza, na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora bila ubaguzi.