Katika maadhimisho ya toleo la 13 la Siku ya Ecobank (Ecobank Day), Benki ya Ecobank Tanzania imeonesha upya dhamira yake ya kushirikiana na jamii za ndani katika kukuza elimu jumuishi na bora kwa wote, ikiangazia kaulimbiu ya mwaka huu “Kuwezesha Kujifunza kwa Ujumuishi kwa Wote.”
Kaulimbiu hiyo inaakisi imani ya Ecobank kwamba kila mtoto, wakiwemo wenye ulemavu, anapaswa kupata fursa sawa ya elimu yenye ubora unaostahili.
Siku ya Ecobank ilizinduliwa mwaka 2013 na imekuwa mojawapo ya programu kuu za uwajibikaji kwa jamii za kundi la Ecobank “Corporate Social Responsibility (CSR)”, ikihusisha wafanyakazi, taasisi ya Ecobank Foundation, na wadau mbalimbali katika kushughulikia masuala muhimu ya kijamii kama afya, elimu na uwezeshaji wa vijana.
Mwaka huu, maadhimisho hayo yamekuwa ya kipekee zaidi kwani yanaenda sambamba na kutimiza miaka 40 ya Ecobank, ikiadhimisha miongo minne ya ubunifu, ukuaji, na kujitolea katika kuendeleza maendeleo ya bara la Afrika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu, amesema kupitia kampeni yetu ya sasa yenye kaulimbiu ‘Kubadilisha Afrika Kupitia Elimu’, Ecobank Tanzania inajivunia kuwanoa zaidi ya watoto 200 katika ujuzi wa kidijitali na akili bandia (AI) kwa kushirikiana na Shule Direct. Tumejitolea kwa vitendo tunatoa mfumo wa usimamizi wa ujifunzaji (Learning Management System) katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, tunasakinisha intaneti ya nyuzi (fibre internet), tunatoa vifaa vya kusaidia kusikia, projector, kompyuta za mezani, na mbao maalum za kufundishia wanafunzi wasioona.
Dkt. Asiedu aliongeza kuwa benki hiyo pia inatoa mafunzo maalum kwa walimu na wanafunzi juu ya elimu ya fedha inayojumuisha matumizi ya teknolojia ya akili bandia ili kuboresha mbinu za kujifunza na kufundisha.
Aidha, mnamo Oktoba 9, 2025, ulifanyika warsha ya mtandaoni ya bara la Afrika (Pan-African Webinar) kwa ushirikiano na Shirika la Global Partnership for Education (GPE) chini ya mada “Je, Teknolojia Inaweza Kuvunja Vikwazo vya Elimu Jumuishi?”
Kikao hicho kiliwaleta pamoja wataalamu, walimu, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), na wazazi kujadili namna teknolojia saidizi na ushiriki wa jamii za ndani unavyoweza kusaidia kujenga mfumo wa elimu ulio sawa, jumuishi na unaowezesha kila mtoto kujifunza bila vikwazo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu akikabidi msaada kwa Mkuu wa Shule Msaidizi – Utawala wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Khadija Omary alieyemwakilisha Mkuu wa Shule Joseph Deo Lugayila wa vifaa vya kusaidia kusikia, projector, kompyuta za mezani, na ubao maalum wa kufundishia wanafunzi wasioona pamoja na kutoa mfumo wa usimamizi wa ujifunzaji (Learning Management System)
Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Ecobank Tanzania, walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa
Mkuu wa Shule Msaidizi – Utawala wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Khadija Omary
alieyemwakilisha Mkuu wa Shule Joseph Deo Lugayila akitoa neno la shukrani kwa Ecobank Tanzania walipofika shuleni hapo kwa ajili ya kutoa msaada ikiwa ni ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Kampuni ya Ecobank wa kutenga siku maalum kusaidia jamii.