Dar es Salaam. Mwigizaji maarufu kwenye tamthilia ya Mpali, Wanga Zulu (51) ambaye kwa Tanzania anafahamika kwa jina la Junza, amefariki dunia.
Junza anayetambulika kama ‘mke mkubwa’ kati ya wake saba wa Mzee Nguzu, kwenye Mpali ya Zambezi Magic, pia anafahamika kama mama Hambe, akiwaongoza wake wenzake kwenye maisha ya shambani.
Kwa mujibu wa mwigizaji mwenzake, Monde aliyewakilisha familia ya Nguzu kwenye msiba huo, alieleza kuwa Junza alifikwa na umauti usiku wa Oktoba 9, 2025 saa tano usiku, baada ya kupatwa na kiharusi akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mafunzo ya Levy Mwanawasa.
Junza ambaye ‘mume’ wake wa kwenye tamthilia ni Nguzu, ameacha mume wake Daniel Mutale na watoto wao watano, ambao wamemwelezea kama si tu mama, bali nguzo ya amani.
Rafiki yake wa karibu na pia mke mwenza wa Nguzu katika tamthilia hiyo, Anna Munamonga (anayefahamika kama Mwiza), alieleza huzuni yake kupitia ujumbe mfupi kwenye Facebook.
Mwaka 2014, Junza alitangaza hadharani kuhusu ugonjwa wa saratani aliogunduliwa nao na safari yake ya kutafuta matibabu, ikiwamo kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo.
Junza amekuwa katika tamthilia ya Mpali akiwa kwenye familia ya Nguzu inayoishi shambani, yenye wake wengi wa rika mbalimbali. Mume wao ndiye muhusika mkuu.
Ndoa hiyo iko kwenye misingi ya ushirikiano wa kifamilia na kibiashara, kiasi cha Junza kuwa na hisa kwenye shamba wanaloishi.
Wakati Nguzu alipofikia umri wa kuoa, familia yake ilimpangia ndoa na Junza, binti wa mmiliki wa shamba la mazao kutoka familia jirani, yenye utajiri na ushawishi sawa na wao.
Baba yake Junza alikuwa na wake wanne, lakini Junza alikuwa mtoto wake wa pekee.
Njia pekee aliyotumi kuhakikisha Junza anapata urithi wake, ilikuwa kwa kuhakikisha anafunga ndoa, ili aweze kuhamishia urithi huo kwa mkwe wake, desturi ya kawaida ya kikabila katika mazingira hayo.
Hivyo basi, Nguzu alijikuta akimiliki utajiri mara mbili, kwa kurithi mali ya baba yake pamoja na ya baba mkwe wake (baba wa Junza).
Hata hivyo, masharti ya ndoa yao yalikuwa kwamba Nguzu angemchukulia Junza kama mshirika sawa wa biashara, katika uendeshaji wa shamba lao.
Masharti haya yalisimamiwa na kushuhudiwa na kukubaliwa na wanachama wote wa familia zote mbili.
Kati ya wake wote, Junza anaonyesha kuwa na moyo wa dhati katika shughuli za shamba. Kama simulizi zinavyosema, yeye ndiye mke wa kwanza alikuwa na Nguzu tangu enzi. Kadri miaka ilivyoenda, ushawishi wake katika shamba uliongezeka kiasi cha kumshawishi Nguzu kusaini mali yote kwake.
Baada ya miaka 17 ya kutengeneza na kuigiza nafasi mbalimbali kwenye televisheni na filamu, Junza alikuwa na sababu ya kusherehekea aliposhinda tuzo ya “Mwanamke Bora katika Burudani na Sanaa” kwenye Tuzo za Push za mwaka 2020, tuzo zilizokuwa na ushindani mkubwa.
Junza ambaye taaluma yake ni ualimu, alicha kazi hiyo na kujihusisha zaidi na uigizaji hali iliyomfanya kupata umaarufu na kushawishi wengine kwenye uigizaji.
Kwenye Mpali ya Zambezi Magic, Junza amekuwa mahili kwenye nafasi anayocheza ya mke mkubwa, kukabiliana na hisia zilizoletwa kwa Nguzu kuongeza wake sita zaidi kwenye familia, na jinsi alivyoigiza kwa mafanikio makubwa tabia mbili tofauti za mke mwema na wakati mwingine adui wa nyumba.
Kufariki kwa Junza bila shaka kutaleta athari kwenye tamthilia hiyo, kwa wanawake waliosalia kila mmoja ana nafasi na haiba tofauti na mwingine.
Mwiza Mike, mwalimu wa Nguzu, huenda ni mke mpendwa zaidi kwa Nguzu. Mwiza daima amekuwa na kibali cha mumewe, na licha ya ushindani wa asili katika nyumba hiyo, wake wengine humvumilia kwa wepesi.
Ingawa naye ana historia ya visa vya ajabu kama alipoamua kuondoka na kuolewa tena, Mwiza daima amekuwa moyo wa familia.
Akipewa kila kitu, huenda akawa mpole na mkarimu, akizingatia kila mtu katika wa ukoo wa Nguzu na matawi yake.
Shuliwe mke mwenye maneno mengi wa Nguzu. Je, kuna mtu anaweza kusema “mwigizaji wa kuchekesha.”
Ingawa ni mtu wa kupendeza, Shupiwe si wa kubezwa. Atatabasamu na wewe, lakini pia anaweza kubadilika ikiwa mipaka yake itavukwa.
Tamara ambaye ni msichana na anaweza kuwa binti wa Nguzu. Kama msemo “nitazame, nimeumbwa kwa ajili ya pesa” ungekuwa mtu, basi huyo mtu angekuwa Tamara.
Vipi tena msichana mpole kama yeye aishie kuolewa na mfanyabiashara mkubwa wa shamba ambaye anaweza kuwa kaka wa baba yake? Sababu pesa, starehe na usalama.
Ukiangalia alivyojihusisha na Hambe, kwa tamaa ya kupata zaidi, na hata kuruhusu wazazi wake wamwoze kwa makubaliano, Tamara yuko kwa ajili ya yeye mwenyewe.
Akipewa usimamizi wa mali ya Nguzu, huenda akaiuza yote kwa anayetoa dau kubwa zaidi, halafu aende kuishi maisha ya kifahari mjini.
Nancy mke mzungu wa Nguzu. Tuzungumze kuhusu asiyehusika moja kwa moja! Nancy hajawahi kuhusika sana katika shughuli za shamba. Kazi yake kubwa ni kupatanisha, na hana haja ya kujua kama ndizi zimeongezeka au kupungua mwaka huu.
Akikabidhiwa usukani, huenda akaamua kuuza kila kitu kama Tamara, kugawana mali na wake wenzake ili kuonyesha utu (labda), na kisha kusafiri, kuvuka bahari bila mpango wa kurudi.
Monde mke aliyekata tamaa. Tukikumbuka vyema, Monde kila mara alijihisi kama hafai kuwa pale. Amejitahidi sana kumpata Nguzu amtazame kwa jicho la kipekee.
Hisia zake za kutothaminiwa zilimpeleka kwenye njia ya giza, na badala ya kupata upendo wa Nguzu kama alivyotarajia, uchawi aliofanyiwa ulikoma haraka na karibu afukuzwe shambani.
Ikiwa atasimama kama kiongozi, huenda akahakikisha shamba linakuwa lake pekee na yeyote atakayebisha, atafukuzwa mara moja!
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.