KINACHOENDELEA Yanga hivi sasa ni kama mtego umewekwa na uongozi wa klabu hiyo kwa benchi la ufundi ambalo mashabiki muda mrefu wamekuwa wakilipigia kelele wakihitaji mabadiliko.
Mtego uliowekwa ni kwa Kocha Mkuu, Romain Folz ambaye inaelezwa hana siku nyingi za kuendelea kuinoa timu hiyo kutokana na presha iliyopo, huku mrithi wake anayetajwa ni Romuald Rakotondrabe maarufu Roro wa Madagascar, kuna kitu kikiendelea. Kilichopo, kuna dakika 180 sawa na mechi mbili ambazo Yanga inakwenda kuzicheza kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers, baada ya hapo, huenda kuna kitu kikatokea.
Katika michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Yanga inahitaji kufika hatua ya makundi, kisha kwenda mbali zaidi ya ilivyokuwa msimu wa 2023-2024, lakini mabosi wa timu hiyo wakikumbuka kilichotokea 2024-2025 walipoachana na Miguel Gamondi kisha timu ikaishia makundi, hawataki kijirudie kwa sasa.
Taarifa kutoka Yanga zinabainisha viongozi wa klabu hiyo wamezisikia kelele za mashabiki kutoridhishwa na namna timu inavyocheza licha ya kutopoteza mechi yoyote ya mashindano msimu huu chini ya Folz na tayari imetetea taji la Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0, Septemba 16, 2025.
Mashabiki wa Yanga wameishuhudia timu hiyo ikicheza mechi tano za mashindano ikishinda nne na sare moja huku ikifunga mabao tisa na kutoruhusu nyavu zake kutikiswa, lakini wanasema hawapati burudani waliyoizoea ya kucheza soka safi na ushindi juu, hivyo wanashinikiza Folz aondolewe.
Kelele hizo zilizidi zaidi Septemba 30, 2025 muda mfupi baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Yanga ilitoka 0-0 na Mbeya City na mashabiki walisikika wakisema: “Hatumtaki, hatumtaki, hatumtaki, aondoke.”
Kutokana na hali hiyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema wamesikia kelele za mashabiki lakini uongozi unaendelea kufanya tathimini na muda ukifika utaamua iwapo itahitajika la kufanya.
“Uongozi unaendelea na tathimini kwa hiki kilichosikika kwa mashabiki, tukubali Sokoine kwa historia umeendelea kuwa mgumu kwetu na mambo mengine yatafanyiwa kazi,” alisema Kamwe.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Mwanaspoti liliripoti taarifa za viongozi wa Yanga kuwa kwenye mazungumzo ya kusitisha mkataba na Folz.
Katika hilo, akatajwa Roro kumrithi Folz, lakini ghafla dili la kocha huyo raia wa Madagascar limeingia utata unaotishia hata ujio wake kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.
Roro ambaye alishamaliza makubaliano katika mambo mengi na Yanga ikiwemo kutumiwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwingine huku mwenyewe akikiri anakuja kuifundisha timu hiyo, lakini utata ambao umeibuka ni namna ya muundo wa benchi lake la ufundi kwani hapo ndipo umeibuka mjadala.
Kitendo cha Roro kutaka kutua Yanga akiwa na watu wawili ambapo wa kwanza ni mmoja wa wasaidizi wake namba moja, lakini changamoto iliyoibuka ni kocha huyo kuwa na leseni ambayo haikidhi matakwa ya kuwa kocha msaidizi, huku Roro mwenyewe akisisitiza huyo ndiye mtu anayemwamini na anataka atue naye nchini.
Lakini, duru kutoka ndani ya Yanga zinadai imemshauri kocha huyo kama hana mtu mwafaka anayekidhi vigezo basi imsaidie kutafuta makocha watatu kisha yeye amchague mmoja.
Hesabu za Yanga pia ni inalenga kumtafutia kocha huyo msaidizi ambaye atamsaidia kwenye lugha ya kuwasiliana na wachezaji wake kwani Roro anajua kuzungumza kwa ufasaha Kifaransa pekee.
Utata wa pili kuhusu dili la kocha huyo ni ishu ya kocha wa mazoezi ya viungo na Roro anataka kuja na kocha wake, lakini viongozi wa Yanga wameridhishwa sana na yule wa sasa Tshephang ‘Chyna’ Mokaila ambaye ni raia wa Botswana.
Mokaila alitua mapema wakati Yanga inaunda benchi la Folz, lakini namna jamaa huyo anavyowapigisha mazoezi wachezaji, kila bosi amegoma jamaa asiondoke.
Wakati hayo yote yakiendelea, Yanga ipo katika kipindi cha takribani siku 12 ngumu za kukabiliana na Silver Strikers katika mechi ya kwanza ugenini hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika maandalizi ya kuelekea mechi hiyo itakayochezwa Oktoba 18, 2025 nchini Malawi, Yanga imekuwa mazoezini tangu Oktoba 6, 2025 ikinolewa na Folz.
Kitendo cha Folz kuendelea kuiandaa Yanga kuelekea mechi hiyo, kinatoa picha ya wazi kwamba uongozi wa klabu hiyo hautaki kumuondoa kwa haraka ili kupima upepo ulivyo.
Yanga imejifunza kilichotokea msimu uliopita na ilimwondoa Kocha Miguel Gamondi baada ya timu kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikampa jukumu Sead Ramovic na matokeo yake timu hiyo ikashindwa kuvuka kwenda robo fainali kurudia rekodi ya msimu wa nyuma yake 2023-2024.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa ndoa ya Yanga na Folz ikaendelea kuwa hai au ikafa kulingana na matokeo ya mechi mbili zijazo za Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu makundi, timu hiyo itakapokabiliana na Silver Strikers ya Malawi. Mechi ya kwanza ni Oktoba 18, 2025 ugenini, marudiano Oktoba 25, 2025 jijini Dar es Salaam.
Wakati presha ya ajira yake ikizidi, Folz amewashtua wachezaji wa timu hiyo wakibaki njiapanda baada ya kubadilishwa mambo.
Kuanzia Jumatatu wiki hii na Folz amerejea kazini, amebadilisha programu nzima ya mazoezi ya timu hiyo ambayo imewaduwaza wachezaji wake.
Mastaa hao wanasema kitu ambacho kilikuwa kinawachanganya kwa kocha huyo, alikuwa na ratiba ya kusimamisha mazoezi na kutoa sana maelekezo, hatua iliyokuwa inapunguza muda wa mpira kupigwa.
Alichobadili Folz ni tangu timu hiyo irejee mazoezini Jumatatu Oktoba 6, 2025, walikutana na mazoezi ya mbio kwa siku mbili za kwanza lakini baada ya hapo wamekuwa wakiucheza mpira zaidi.
Wakati Folz anasikilizia hatima yake, kuna vichwa nane ambavyo vina kauli ya mwisho ya kuamua mabadiliko ya benchi hilo la ufundi.
Vichwa hivyo nane ndiyo vinaunda Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Yanga ambayo ndio chombo chenye mamlaka ya kuajiri au kuachana na makocha wa timu hiyo.
Vigogo hao nane wanaongozwa na Rais wa klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said ambaye katika miaka ya hivi karibuni ameonyesha nguvu kubwa ya ushawishi katika masuala ya usajili wa wachezaji na ajira za makocha na maofisa wa benchi la ufundi. Kichwa kingine ni Arafat Haji ambaye ni Makamu wa Rais wa Yanga.
Ukiondoa vigogo hao wawili, kuna Wajumbe wa Kamati ya Utendaji sita ambao ni Gerald Kihinga, Seif Gulamali, Munir Seleman, Alex Ngai, Yanga Makaga na Rodgers Gumbo.