Tumbi yakabiliwa na upungufu wa watumishi, Serikali yatoa kauli

Kibaha. Wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi) ikiadhimisha miaka 58 tangu kuanzishwa kwake, changamoto za upungufu wa watumishi na ukosefu wa uzio zimeendelea kuibua hofu kuhusu ufanisi na usalama wa hospitali hiyo, huku wagonjwa wakisifu huduma bora zinazotolewa licha ya changamoto hizo.

Akizungumza leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 wakati wa kilele cha maadhinisho hayo Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Amani Malima, amesema kwa sasa hospitali ina jumla ya watumishi 497 pekee kati ya mahitaji ya 680, hali inayosababisha mzigo mkubwa wa kazi kwa waliopo.

“Tunajitahidi kutoa huduma bora, lakini upungufu wa watumishi ni changamoto kubwa. Tunapokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Bagamoyo, Kibaha, Dar es Salaam na Rufiji, hivyo mahitaji ya huduma ni makubwa,” amesema Dk Malima.

Ameongeza kuwa ukosefu wa uzio unaozunguka hospitali hiyo imekuwa kero ya muda mrefu na unahatarisha usalama wa mali na watumishi.

Pamoja na changamoto hizo, Dk Malima alitaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 58, ikiwemo kuboresha huduma za kibingwa kwa wagonjwa wa mifupa, macho, afya ya uzazi, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na huduma za wagonjwa wa ndani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Serikali itashirikiana na Wizara ya Afya kutatua changamoto hizo kwa hatua.

“Hospitali ya Tumbi ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa mkoa huu, Serikali ya Mkoa itaendelea kushughulikia changamoto za rasilimali watu na miundombinu ili huduma zibaki kuwa bora zaidi,” amesema Mnyema.

Kwa upande wao, baadhi ya wastaafu waliotumikia hospitali hiyo kwa zaidi ya miaka 35, akiwemo Grace Mwaimu na Hanis Ismail, waliwataka watumishi waliopo kuendelea kufanya kazi kwa maadili na moyo wa kujitolea.

“Tulifanya kazi kwa upendo na heshima, na tunaamini kizazi kinachoendelea kitadumisha moyo huo kwa manufaa ya wananchi,” amesema Mwaimu.

Wagonjwa waliokuwa wakipata matibabu hospitalini hapo nao hawakusita kusifia huduma wanazopokea.

Zaituni Rajabu, mkazi wa Mlandizi, amesema: “Huduma zimeboreshwa sana, wauguzi wanatoa ushirikiano na madaktari wanatuelezea vizuri hali zetu. Hata kama foleni ipo, wanatuhudumia kwa upendo.”

Naye Ally Mussa, mkazi wa Kibaha, amesema Tumbi imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini.

“Nilitibiwa hapa bure wakati wa kambi za matibabu ya kibingwa, walinirudisha afya yangu. Hii hospitali inastahili pongezi,” amesema Mussa.

Dk Malima alihitimisha kwa kueleza kuwa hospitali hiyo inaendelea kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuongeza wigo wa huduma za kibingwa, kuimarisha miundombinu na kufungua vitengo vipya vya huduma za uchunguzi na tiba.

“Mpango wetu ni kuona Tumbi inakuwa kitovu cha huduma za kibingwa ukanda wa Pwani, tukijikita zaidi katika teknolojia ya kisasa na huduma rafiki kwa wagonjwa,” alisema Dk Malima.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na watumishi, wastaafu, wagonjwa na wadau wa afya, ambapo pia hospitali ilitambua michango ya taasisi na mashirika yaliyoshirikiana nayo kuboresha huduma kwa wananchi.