Mzee wa miaka 75 ajinyonga, aacha maswali

Rukwa. Mzee Jelas Lunguya mwenye umri wa (75) mkazi wa Kijiji Cha Nchenje kata ya Kate wilayani Nkasi mkoani Rukwa amefariki dunia baada ya kujinyonga.

‎Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mtendaji wa kijiji cha Nchenje Salome Auseni amesema kuwa  tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Ijumaa ambapo mzee huyo alikutwa amefariki kwa kujining’iniza kwenye mti kwa kutumia kamba ya katani.

‎Amedai kuwa mti huo alioutumia kujinyonga upo nje kidogo ya nyumba yake na unajulikana kwa jina la mchese na hadi sasa haijulikani chanzo Cha tukio hilo.

‎Mtendaji huyo amefafanua kuwa tukio hilo la mzee huyo kujinyonga limeacha maswali mengi kwa jamii na familia yake kwa maana kwamba hawajawahi kusikia mgogoro wowote wa kifamilia ambao unaweza  kupelekea mtu kuchukua maamuzi magumu Kama hayo.

Baadhi ya majirani wa marehemu akiwemo Teonas Fwamba amesema kuwa mzee huyo alikuwa sio mzungumzaji na inawezekana alikuwa na changamoto iliyokuwa inamsibu.

“Kwa kweli huyu mzee sio mzungumzaji na inawezekana kuna jambo lilikuwa linamtatiza na alikuwa hasemi hivyo kuna la kujifunza ukiwa na jambo washirikishe watu ili wajue namna ya kukusaidia,” amesema fwamba

‎Afisa mtendaji amesema kuwa marehemu amezikwa baada ya taratibu za kipolisi kukamilika.

‎Mkuu wa wilaya Nkasi, Peter Lijualikali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa uchunguzi zaidi unaendelea juu ya tukio hilo.