Heche aibua historia ya Mabere Marando kwa kumtembelea nyumbani

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), John Heche amefanya ziara maalumu ya kumtembelea aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Mabere Marando.

Heche amefanya ziara hiyo leo Jumamosi, Oktoba 11, 2025 akiwa na viongozi wenzake kumtembelea Marando ambaye ni miongoni mwa waasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini.

Marando ambaye alianzia kwenye chama cha NCCR-Mageuzi kilichokuwa na idadi kubwa ya wanasheria na baadaye kuhamia Chadema, amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema, ziara hiyo imelenga kutambua na kuthamini mchango wa viongozi waliotangulia, sambamba na kuimarisha mshikamano wa ndani ndani ya chama.

Mabere Marando ni mwanasheria na mwanaharakati wa siasa nchini Tanzania, anayejulikana kwa mchango wake katika harakati za kuanzisha mfumo wa vyama vingi nchi nzima.

Alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasia katika kipindi cha mwisho wa mfumo wa chama kimoja.

Vuguvugu la mageuzi ya kisiasa lilianza kuwa na sauti nchini Tanzania katikati na mwishoni mwa miaka ya 1980, sehemu ya kukua kwa mashinikizo ya watu wanaotaka mabadiliko ya kikatiba na mfumo wa vyama vingi.

Mabere Marando alikuwa mmoja wa wanaharakati vijana walioko mstari wa mbele miongoni mwa watu kama Ndimara Tegambwage, Prince Bagenda na Mashaka Chimoto.

Mkutano wa vuguvugu la mageuzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam mwaka 1991, vijana na waasisi wa mageuzi walikusanyika kuunda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (National Committee for Constitutional Reform, kwa kifupi NCCR), ambayo baadaye iligeuka kuwa chama cha NCCR-Mageuzi.

Katika kamati hiyo, Chifu Abdallah Fundikira aliteuliwa kuwa Mwenyekiti na Mabere Marando aliteuliwa Katibu.

Kamati hiyo iliendelea na mikakati ya harakati za mageuzi ikihusisha wadau mbalimbali; wanachama wa kamati hiyo walitembelea maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu kuhusu vyama vingi na umuhimu wake.

Hatimaye, mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi uliruhusiwa rasmi na chama kilichotokana na harakati hizo kikajulikana kama NCCR‑Mageuzi huku Marando akiwa miongoni mwa waanzilishi wake.

Mwaka 1992 Marando alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa muda NCCR-Mageuzi na mwaka 1994 aliidhinishwa rasmi ikiwa ni moja ya hatua za kuendeleza mapambano waliyoanzisha.

Hata hivyo, mwaka 1995 mara baada ya Augustine Mrema kuhama CCM, uongozi wa NCCR-Mageuzi ulishauriana na kumkaribisha na kumpa uongozi wa kuwa mwenyekiti wa taifa ili kuongeza nguvu ndani ya NCCR-Mageuzi na Marando akawa Katibu Mkuu wa chama, akisaidiwa na viongozi wengine kama Prince Bagenda na Ndimara Tegambwage.

Marando mwaka 2010, alihamia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako alikuwa mwanasheria wa chama na alishika nyadhifa zingine ikiwamo ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.