Majaliwa atoa maagizo sita kuelekea Dira ya Taifa 2050

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameainisha mikakati ya Serikali kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa, 2050 kwa kutoa maagizo sita muhimu.

Majaliwa ametoa maagizo hayo sita kwenye kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambalo limefanyika leo Jumamosi, Oktoba 11, 2025, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (udsm) likiwa na kauli mbiu “Nguvu Kazi Yenye Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa: Kuendeleza Urithi wa Mwalimu Nyerere kuelekea Dira 2050.”

Akiwa mgeni rasmi  kwenye kongamano hilo akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo sita muhimu katika kuwezesha kufikiwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa, 2050.

“Falsafa ya Mwalimu Nyerere katika elimu ni nyenzo muhimu katika kufikia Dira 2050. Katika Elimu Baba wa Taifa aliamini elimu ni chombo cha kumkomboa mwanadam kiuchumi, kimaadili na kijamii,” amesema Waziri Mkuu.

Kwanza, ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na  Mafunzo Stadi (NACTVET) kuboresha mitaala ya elimu ili ijibu mahitaji ya sasa ya jamii na soko la ajira, na kuandaa wahitimu wabunifu wanaoweza kutatua changamoto za kijamii.

Agizo la pili, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya elimu na taasisi za ujuzi kwa kuboresha mitaala, kupanua vyuo vya VETA, kuongeza ufadhili wa elimu ya juu na kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga nguvu kazi ya kisasa yenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Majaliwa ambaye alikuwa akizungumza kwa msisitizo ametoa agizo la tatu kwa kuitaka sekta ya viwanda kuanzisha vituo vya mafunzo, utafiti na ufadhili wa teknolojia kwa ajili ya kuongeza ajira na ujuzi wa vitendo kwa vijana.

Pia, agizo la nne  ameliekeza Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuimarisha elimu ya uraia ili kujenga kizazi chenye maadili, uzalendo na kuheshimu dira ya Taifa.

Akizungumzia agizo la tano, amevitaka vyuo vikuu kama Chuo Kikuu cha DaresSalaam (Udsm), Chuo Kikuu cha  Dodoma (Udom) na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) kuendeleza tafiti na bunifu zitakazotoa majibu ya changamoto za sasa kama ajira, teknolojia na mabadiliko ya tabianchi.

Agizo la sita, amehimiza ushirikiano mkubwa kati ya serikali na sekta binafsi katika kuibua na kukuza fursa za ajira na uwekezaji akisema sekta binafsi ni injini muhimu ya uchumi na haiwezi kuachwa nyuma katika utekelezaji wa Dira 2050.

Majaliwa akitambua umuhimu wa mjadala wa fikra za Mwalimu, amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeendelea kuwa taasisi imara katika kuchochea fikra na tafakuri za maendeleo, kikienzi urithi wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa Taifa.

Amesisitiza kuwa falsafa za Mwalimu kuhusu maendeleo na elimu ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa 2050, akisema kuziunganisha na hali halisi ya sasa kutasaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Majaliwa amesema katika falsafa ya Mwalimu, elimu ni chombo cha kumkomboa mwanadamu kiuchumi, kimaadili na kijamii, hivyo kuenzi fikra hizo ni kuwekeza katika elimu inayojenga jamii yenye maarifa, ujuzi, ubunifu na maadili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Alexander Makulilo amesema lengo la kongamano hilo ni kukuza mijadala na mageuzi ya elimu kwa ajili ya kuendeleza urithi wa Mwalimu na kuchochea nguvu kazi ya Taifa kuelekea Dira 2050.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema maadhimisho hayo ni jukwaa la kutafakari maono ya Mwasisi wa Taifa katika ujenzi wa jamii yenye maarifa, ujuzi na uzalendo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Viwanda na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Dira 2050 imeweka rasilimali watu kama nguzo kuu ya maendeleo, akibainisha kuwa asilimia 76 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35, hivyo ni muhimu kuwekeza katika elimu na ujuzi.

Amesema kufikia Juni 2025, Tanzania ilikuwa na laini za simu milioni 92 kutoka milioni 55 mwaka 2015 na zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma ya intaneti, jambo linaloonesha ukuaji wa teknolojia unaohitaji elimu ya kisasa.

Amesema Mwalimu Nyerere aliwahi kusisitiza kuwa elimu ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya ukandamizaji na akamnukuu aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, akisema: “Ili jamii ipate maendeleo inahitaji mambo matatu: kwanza elimu, pili elimu, na tatu elimu.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, David Kafulila amesema sekta binafsi ina wajibu mkubwa wa kutoa mitaji, teknolojia na fursa za ubunifu kufanikisha Dira 2050 na kwamba serikali pekee haiwezi kufanikisha dira hiyo bila ubia wenye tija.

Kongamano hilo limebeba ujumbe wa kuendeleza urithi wa Mwalimu Nyerere kupitia elimu, ujuzi na maadili, likisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu kama nyenzo ya maendeleo na demokrasia kwa mustakabali wa Taifa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake  Tanzania (WCC), Dk Mwajuma Hamza, amesisitiza uwekezaji katika tafiti za kitaalamu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika kuwezesha wanawake wenye ujuzi kushiriki kikamilifu katika kufikiwa malengo ya Dira 2050.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji kikamilifu wa sekta binafsi katika kutoa mafunzo ya vitendo kwa vijana ili kuchochea uwezo wa ujuzi na maarifa katika kuandaa nguvu kazi ya Taifa.

“Ushirikiano na sekta binafsi kwakuweka vivutio vya kikodi tutawezesha sekta binafsi kuwekeza na kutoa mchango wake katika kupika vijana kiujuzi na maarifa zaidi ili waweze kutumika katika mipango mbalimbali ya Dira 2050,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Sabath Nyamsenda, akizungumzia nafasi ya elimu katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, amesisitiza vyuo vikuu vijikite katika kutoa elimu inayojenga wasomi wenye uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo ili kupata rasilimali watu inayohitajika kuvusha Taifa.

“Hatuwezi kufanikiwa ikiwa vyuo vikuu vitaacha kuzalisha vijana wasomi aliowataka Mwalimu Nyerere, wenye uwezo wa kuhoji na kataa mifumo kandamizi ili kuweza kufikia fursa zenye staha tofauti na kuwa na mifumo mibovu ya ajira kandamizi zisizo na staha,” amesema.