Spika Zanzibar aeleza siri ya kukua kwa uwekezaji visiwani hapo

Unguja. Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid amesema sheria nzuri zinazotungwa zimeendelea kuvutia kampuni kubwa za biashara kuwekeza Zanzibar, hatua inayotajwa kuleta mchango wa ukuaji wa uchumi wa visiwa hivyo.

Amesema Baraza la Wawakilishi na Serikali wataendelea kufanya kazi kuhakikisha kuna mazingira ya uwazi, yanayofaa kwa biashara huku wakilinda watumiaji, wafanyakazi na mazingira.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 11, 2025 wakati wa kuzindua duka kubwa la vifaa vya kielektroniki ya Hisense linalomilikiwa na Kampuni ya Electronic Hub.

“Kwa sasa kuna sheria nzuri za uwekezaji, na tutaendelea kuhakikisha sheria zinakuwa bora zaidi kuendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi kwa masilahi mapana ya uchumi wa nchi yetu,” amesema.

Mbali na sheria, pia Spika Zubeir amesema kuna sera nzuri zinazovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Tunawakaribisha wawekezaji ambao huleta si tu mtaji, bali pia mazoea mazuri yua kuheshimu sheria, kuajiri, kujenga uwezo na uwajibikaji wa kijamii,” amesema

Akizungumza kuhusu duka hilo, Zubeir amesema ni kuendana na mpango wa Serikali kuondokana na uingizwaji wa vifaa visivyo na ubora na hivyo kulinda mazingira.

“Hivi vifaa vinatumia umeme kidogo na vinaendana na mazingira kwa sababu ya uchakavu,” amesema.

Amesema wataweka kanuni pia za kuwalinda watumiaji, iwapo yataibuka malalamiko kutokana na vifaa visivyo na ubora.

“Uwekezaji wa namna hii unakaribishwa, tumezoea kutoka katika maduka ya kawaida, unanunua kitu cha thamani lakini baada ya mwaka kinakuharibikia, vitu vingi tunavyonunua havina waranti, ila hapa unapewa zaidi ya mwaka,” amesema Zubeir.

Naye Mkurugenzi wa Electronic Hub, Naeem Sikandar amesema dhamira ya kuwekeza Zanzibar ni kuongeza mchango katika uchumi wa visiwa humo na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa taifa na kuwaletea wananchi huduma bora zaidi.

“Kuwapo kwa Hisense kunaleta taswira mpya ya Zanzibar kama eneo rafiki kwa teknolojia na biashara, hivyo kufungua milango kwa uwekezaji zaidi wa kielektroniki.

Naye Naibu meneja Mkuu wa Hisense Afrika Kusini, Luna Nortje amesema Zanzibar ina nafasi ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki, akisema kuwapo kwa bidhaa hizo ni sehemu ya kukuza mkakati huo kibiashara.

Uzinduzi wa duka hilo, itachochea ajira kwa vijana 100 moja kwa moja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu wa ndani ya nchi.