Moto wateketeza vyumba 12 vya makazi ya watu Moshi

Moshi. Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza vyumba 12 vya makazi ya watu pamoja na vyumba viwili vya biashara katika Mtaa wa Dar es Salaam Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema tukio hilo  limetokea leo Oktoba 11, 2025 na kwamba hakuna madhara ya kibinadamu zaidi ya kuteketeza  mali zilizokuwemo ndani.

“Leo tulipokea taarifa ya tukio la moto katika Mtaa wa Dar es Salaam, Kata ya Kiusa, Manispaa ya Moshi, tulifika eneo la tukio na tulikuta moto umesambaa na vyumba 12 vya makazi ya watu vimeteketea kwa moto na vyumba viwili vya biashara,” amesema Kamanda Mkomagi na kuongeza;

“Wakati tukio linatokea hakukuwa na mtu ndani kulikuwa na watoto wadogo wawili ambao baada ya kuona moto walikwenda kwa jirani kutoa taarifa na majirani waliweza kutupa taarifa na tuliweza kufika eneo la tukio.”

Aidha, amesema wamefanikiwa kudhibiti moto huo kutoenea kwenye nyumba nyingine za jirani baada ya kuongezewa nguvu na zimamoto kutoka kiwanda cha sukari cha TPC.

“Moto ulikuwa umesambaa kote bahati nzuri,  tumefanikiwa kudhibiti moto na kuokoa nyumba nyingine za jirani ambazo zingeweza kushika moto,” amesema Kamanda Mkomagi.

Akizungumza shuhuda wa tukio hilo, Lightness Meada amesema moto ulikuwa ni mkubwa na kwamba walishindwa kudhibiti licha ya kutumia nguvu za ziada mpaka zimamoto walipofika.

“Tulikuwa tumekaa  nje  gafla akaja mtoto akasema kuna moto kule kwetu, tukatoka hapa tukaenda tukakuta moto umesambaa nyumba nzima.

“Moto ulizidi na hakuna kitu hata kimoja kilichookolewa, tumepambana kuuzima lakini hatukufanikiwa chochote moto ulikuwa ni mkubwa sana,” amesema.