Rombo. Mgogoro wa ardhi kati ya familia ya Mzee Peter Morris Shirima na Kanisa Katoliki Parokia ya Mtimhoo, Wilaya ya Rombo, umechukua sura mpya baada ya serikali kupitia Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro, Rehema Mdee, kueleza kuwa, familia hiyo ilishalipwa fidia na kupewa ardhi mbadala tangu miaka ya 1970.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya familia ya Morris kufika eneo la Kanisa la Mtimhoo, Kijiji cha Msaranga, wilayani Rombo na kufanya ibada za kimila wakidai kurejea kwenye ardhi ya mababu zao.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 4, 2025 ambapo mzee Morris akiwa na familia yake ya watu zaidi ya 10, walifika eneo hilo wakiwa wamejifunga vitambaa vyeupe mikononi na shingoni huku wakiwa wamebeba pombe ya kienyeji (mbege), ulezi na mbuzi mweupe waliokusudia kumtumia katika ibada yao ya kimila.
Morris alisimama barabarani anakoamini waumini hupita kuelekea kanisani, akaotesha migomba na kumimina ulezi kwa kutumia kijiko cha mbao (kipao) huku akigeuka pande zote na kutamka maneno kwa lugha ya Kichagga huku akiinywa mbege na kunuia akidai anazungumza na Mungu wake.
Tukio hilo liliwastua waumini na viongozi wa kanisa, akiwemo kiongozi wa kanisa hilo, Padre Benedict Kagwa, ambaye alilazimika kutoka kushuhudia na kuomba msaada wa polisi baada ya kuona familia hiyo ikijenga kibanda cha muda na kuendelea na shughuli nyingine.
Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Rombo, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP) Leonard Kambwa, walifika eneo hilo na kuwataka kuacha shughuli hizo mara moja.
“Kuna haja ya ninyi kutumia busara. Kitendo kilichofanyika hapa si kizuri, kinachochea taharuki isiyokuwa na maana. Kuanzia leo tunahitaji wahusika wa pande zote mbili walete vielelezo vyao na upande wa kanisa nao wataleta zao, kisha tutachekecha. Inawezekana tusiwe wa mwisho kutatua huu mgogoro, tutaupeleka katika hatua nyingine zinazofuata,” alisema OCD Kambwa.
Akizungumza leo Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro, Rehema Mdee amesema familia ya Morris mara kadhaa imekuwa ikitoa malalamiko hayo, lakini kumbukumbu za Serikali zinaonyesha walishalipwa fidia na kupewa shamba jingine.
“Kanisa lipo pale kwa zaidi ya miaka 30. Familia ya Morris ilifidiwa fedha na ardhi mbadala katika eneo la Kirachi na wamelitumia eneo hilo kwa shughuli zao. Si kweli kwamba bado hawajawahi kufidiwa,” amesema Mdee.

Jengo la kanisa katika lililosimamishwa kuendelea na ujenzi kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya familia ya Peter Morris na Kanisa katoliki Jimbo la Moshi Parokia ya Mtimhoo.
Amefafanua kuwa mwanzoni mwa mwaka huu familia hiyo ilipewa nafasi ya kueleza madai yao mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Ardhi na Maliasili wakati wa kikao cha hadhara kilichofanyika Rombo na yakatolewa majibu.
“Nilishuhudia mwenyewe pale. Mzee Morris alikuwa na bango akinyanyua, akapewa nafasi kuzungumza, lakini wananchi waliokuwepo walimkana hadharani. Hata nyaraka tulizonazo zinaonyesha alishalipwa kiasi cha kama Sh5,000 tangu miaka ya 1970. Suala hili limeshajadiliwa mara nyingi, tatizo ni kutokukubaliana na maamuzi yaliyokwishatolewa,” amesema.
Kamishna huyo ameongeza kuwa nchi inatawaliwa kwa sheria na si kwa maamuzi ya mtu binafsi, akisisitiza kuwa hatua ya kuvamia kanisa na kufanya ibada za kimila si suluhu ya mgogoro.
“Njia sahihi ni kufuata taratibu za kisheria. Kama mtu anaona bado hajapata haki, aende mahakamani badala ya kuchochea taharuki kwenye maeneo ya ibada,” ameongeza Mdee.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Vikar wa Jimbo Katoliki Rombo, Padre Amedeus Mtui, amesema kuwa Kanisa halina uhusiano wa kisheria na familia ya Morris, bali makubaliano yaliyo halali ni kati ya Kanisa na Kijiji cha Mtimhoo.

Mzee Peter Morris Shirima akifanya ibada ya kimila kwenye eneo la mgogoro kati yake na Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi Parokia ya Mtimhoo, Rombo. Picha na Yese Tunuka.
Padri Mtui amesema wameshangazwa kuona baadhi ya watu wakianza shughuli zao katika eneo hilo, ilhali eneo limekabidhiwa Kanisa kwa utaratibu rasmi wa kijiji.
Amebainisha kuwa mkataba wa ardhi hiyo ulitolewa baina ya kijiji na Kanisa na kwamba hawajawahi kuingia makubaliano yoyote na familia inayodai shamba hilo.
“Sasa, baada ya miaka mingi ya amani na maendeleo, familia hiyo inadai kuwa shamba ni lake. Tumeshauriwa kuwasilisha vielelezo vya kikao cha kijiji na fidia iliyotolewa mwaka 1980,” amesema
“Eneo hili tulipewa na kijiji kwa makubaliano rasmi. Hatukuwahi kuingia makubaliano na familia ya Morris. Kijiji kililipia fidia kwa fedha na shamba jingine. Kwa hiyo, kama bado wanadhani hawajapatiwa haki yao, wapeleke mahakamani,” ameongeza.
Padre Mtui amefafanua kuwa eneo hilo limeendelezwa kwa amani kwa miongo kadhaa, likiwa na makazi ya muda mrefu na kupewa hadhi ya parokia.
“Kanisa tayari limeanza hatua za kisheria kwa kuripoti polisi na kukusanya vielelezo vyote vinavyohusiana na mkataba wa awali na fidia. Hatuhitaji mtu yeyote kuingilia amani au shughuli za Kanisa. Tutafuata taratibu za kisheria kuhakikisha haki inatendeka,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa maeneo ya kijamii mara nyingi hutatuliwa kwa makubaliano ya kijiji, ambapo wanakijiji hushirikiana kujenga shule, zahanati, au kanisa.
Kwa upande wake Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Moshi, Gastor Temu, amesema: “Mgogoro ninaufahamu na nafikiri wameshalishughulikia vizuri.”
Akizungumza na Mwananchi katika eneo ulipotokea mgogoro, familia ya Mzee Peter Morris ilidai Kanisa Katoliki limechukua eneo walilopewa na baba yao kwa mgongo wa upanuzi wa shughuli za maendeleo ya shule ya msingi Mtimhoo tangu miaka ya 1970.
Familia hiyo inadai kuwa eneo hilo lilikuwa na nyumba zisizopungua tatu za misonge na kaburi la familia, lililopo hadi sasa karibu na kanisa.
Mzee Morris amedai kuwa mwaka 1980 alipokea barua ya “stop order” kutoka ofisi ya kijiji ikiwazuia kuendelea na shughuli za kilimo na ujenzi, na baadaye kamati ya ulinzi na usalama ya Rombo iliketi na kumtaka aondoke katika eneo hilo.
Familia hiyo inasema walichukuliwa eneo hilo kwa madai ya upanuzi wa shughuli za umma, huku Mzee Peter Morris ambaye ni baba wa watoto 10 akibainisha kuwa shamba hilo lilikuwa tayari limechangia maendeleo ya shule na barabara ya hatua sita.
Mzee Morris ameeleza kuwa fedha zilizotolewa kama fidia hazikumridhisha, na kwamba licha ya kuandika barua kwa Willium Lukuvi (Waziri wa Ardhi wakati huo) na kuambiwa Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Kilimanjaro afuatilie kesi hiyo, hajapata mrejesho wowote kwa miaka sita sasa.
Familia hiyo imesema kuwa wiki kadhaa zilizopita waliitwa kwenye kamati ya usuluhishi ambapo walikutana na padre na wajumbe wake, lakini hawakupata muafaka.
Aidha familia hiyo imeiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kuupatia suluhu ya kudumu na kuwezesha haki kupatikana.
Kwa mujibu wa familia ya Morris mgogoro huo ulianza mwaka 1970 baada ya Serikali ya kijiji cha Msaranga kuchukua maeneo kutoka kwa familia kadhaa kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule.
Familia ya Morris inadai ilikuwa miongoni mwa walioondolewa na kulipwa fidia. Miaka ya 1980 walipewa barua ya stop order wakizuiwa kuendelea na kilimo eneo hilo, na baadaye sehemu hiyo ikaendelezwa na Kanisa Katoliki.
Kwa zaidi ya miaka 30 eneo limekuwa likitumiwa na Kanisa Katoliki hadi likapata hadhi ya Parokia. Licha ya fidia hiyo, familia ya Morris imeendelea kudai eneo hilo wanalodai ni haki yao, wakisema walinyimwa ardhi kinyume cha makubaliano, wakati serikali na kanisa zikisisitiza walifidiwa kwa mujibu wa sheria.