Mbeya. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ally Ussi amesema ameridhishwa utekelezaji wa uboreshwaji na upanuzi wa mradi wa maji Kata ya Ipinda Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya, huku akimtaja Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuiheshimisha Serikali.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh705 milioni utakao hudumia wananchi 10,000 kwa siku ambao unatekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya -Uwsa), kwa ufadhiri wa fedha za Mfumo waTaifa wa Maji.
Ussi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 11,2025 wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Kata ya Ipinda Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya, ambao utaondoa adha kwa wananchi na kumtua Mama ndoo kichwani.
“Wizara ya Maji ni miongoni mwa wizara zilizofanikiwa chini ya usimamizi wa Kaka yetu mweledi Jumaa Aweso kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kwa kushirikiana na watendaji wa Mamlaka ya Maji Mbeya na wenzetu wa Ruwasa,”amesema.
Amesema katika mikoa 193 ambayo mbio za mwenge wa uhuru kitaifa umepita Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imefanya vizuri katika usimamizi jambo ambalo limeleta heshima kubwa kwa Wizara ya Maji chini ya Serikali ya awamu ya sita.
“Mamlaka ya Maji Mbeya na wenzetu wa Ruwasa kwa kweli wanaendelea kuheshimisha Wizara ya Maji naamini ujio wa mwenge wa uhuru ni ishara ya kuonyesha jinsi gani wana Ipinda wana ondokana na changamoto ya miundombinu ya maji safi na salama,”amesema.
Katika hatua nyingine ametaja sababu za ujio wa Mwenge wa Uhuru ni jambo kubwa na hakuna mahala uendako pasipo kuwepo matumaini ,upendo na heshima baina ya viongozi wa Serikali vyama vya kisiasa na kidini ambao wako kwenye maeneo husika.
“Ni jukumu letu kupitia kauli mbiu ya mwenge wa uhuru kwa kila Mwananchi kutimiza wajibu wake kikatiba,kidemokrasia katika taifa hili,lakini kuwakumbusha duniani hakuna nchi ambayo haiendeshwi kwa mujibu wa katiba na sheria inayo simamiwa “amesema
Ussi amesema Tanzania inajivunia katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 42 kifungu cha (2) mstari wa 65 inasema Tanzania itaweza kufanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano.
Amesema kwa upande wa Tanzania bara tutaenda kuchagua Rais, wabunge na madiwani na kuomba wananchi wa Ipinda Wilaya ya Kyela kupitia hamasa ya mapokezi ya mwenge wa uhuru pia wajitokeze kwenye uchaguzi mkuu kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani .
“Niwatake Oktoba 29,2025 nendeni mkapige kura kwa wingi katika maeneo yetu twendeni tukamchague Samia tukajenge imani naye amefanya mambo mengi,lakini wananchi mtarajie kuona uwepo wa maboresho ya miundombinu ya elimu,afya,maji katika miji na vijijini,”amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Kyela , Mhandisi Raphael Kolong’oyo amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya M/s Scorpion Limited ya jijini Dar es Salaam.
Amesema mpaka sasa umefikia asilimia 32 na amelipwa Sh222 milioni kati ya fedha za mradi zaidi ya Sh 705 milioni.
” Awali Kata ya Ipinda ilikuwa na mradi wa Kanga group uliojengwa mwaka 1980 ,lakini baada ya mamlaka kuona ongezeko la watu ililazimika kubuni mradi wa uboreshwaji na upanuzi wa huduma ili kukidhi ongezeko la huduma na upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu,”amesema.
Ameongeza uboreshwaji wa huduma ya maji Ipinda ulisanifiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mbeya -Uwsa ), kwa upande wa Wilaya ya Kyela na Kasumuru mwaka 2022,2023 na kuanza utekelezaji mwaka 2023, 2024,” amesema.
Amesema utaondoa hadha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ikiwa ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya kutaka asilimia 85 ya watanzania kufikishiwa huduma hiyo muhimu na kumtua Mama ndoo kichwani.
Mmoja wa Mama lishe Anitha Elius amesema wanashukuru Serikali kwa kuleta mradi huo kwani awali walikuwa wakihaha kusaka huduma hiyo na kununua kwa ndoo ya lita ishirini kwa Sh500 hadi Sh1,000.