Waliotembea kilomita 70 kufuata huduma kujengewa kituo cha afya

Same. Serikali imetoa zaidi ya Sh629 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Vunta, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Zaidi ya wananchi 13,000 kutoka kata za Vunta na Kirangare wamekuwa wakilazimika kutembea zaidi ya kilomita 70 kufuata huduma katika Kituo cha Afya cha Hedaru na Hospitali ya Wilaya ya Same kutokana na ukosefu wa kituo cha karibu.

Akizungumza leo, Jumamosi Oktoba 11, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya vijijini, hasa katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za haraka kutokana na umbali kutoka vituo vilivyopo.

“Kukamilika kwa Kituo cha Afya cha Vunta kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, zikiwemo huduma za kibingwa,” amesema Mgeni.

Amesema ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika Desemba 31 mwaka huu, na hivyo kuondoa adha hiyo kwa wananchi wa maeneo hayo.

Aidha, amewataka wasimamizi wa mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo haya ya milimani, hasa Kata ya Vunta na jirani zake. Ongezeni kasi ya ujenzi ili wananchi waanze kunufaika, maana kwa sasa wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 70 na kutumia gharama kubwa za usafiri kufuata huduma Hedaru au Hospitali ya Wilaya ya Same,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Vunta, Thomas Kalinga amesema mradi huo utaboresha mazingira ya utoaji huduma na kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi ambao walikuwa wakichelewa kupata huduma kutokana na umbali mrefu.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu, kwani utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Kata ya Vunta na maeneo jirani,” amesema Kalinga.

Mmoja wa wananchi wa Kata ya Vunta, Donatha Mdee, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya za karibu, hali iliyowalazimu kutumia gharama kubwa kutafuta huduma hizo.

“Tunaishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Vunta. Tumeteseka kwa miaka mingi; ukiwa na mgonjwa amezidiwa, kumfikisha hospitalini ni changamoto kubwa kutokana na umbali na gharama za usafiri, achilia mbali gharama za matibabu,” amesema.

Naye Hassan Mdee, mkazi wa Same, ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma karibu na makazi ya wananchi, akisema hatua hiyo itapunguza mateso waliyokuwa wakipitia kwa muda mrefu.