Dar es Salaam. Mwanasaikolojia mashuhuri, Alfred Adler, aliwahi kueleza tabia za watu ndani ya familia.
Aligundua kuna uhusiano wa karibu kati ya tabia za mtu na uzao wake katika familia kama ni wa kwanza au wa mwisho.
Alisema, suala la umezaliwa wa ngapi huja na matarajio fulani na namna wazazi wanavyohusiana na wewe, hali inayoweza kuathiri tabia zako.
Akiizungumzia nadharia hii ya Adler, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Christian Bwaya anasema inaakisi tabia za wazazi na matarajio kwa watoto na namna ambavyo zinaathiri ukuaji wao.
“Tukijitahidi kuondoa upendeleo, kuwachukulia watoto kuwa na hadhi sawa, kuwafanya wajione wana thamani inayofanana, hizi tofauti ya tabia zinazotokana na nafasi ya mtoto kwenye uzao hazitakuwepo,” anasema.
Hivi sasa kuna sintofahamu, baadhi ya watu wakiamini mzaliwa wa kwanza ni kiongozi, hubeba majukumu wa wadogo zake huku mzaliwa wa mwisho akiwa mtu wa kudekezwa.
Wapo wanaopingana na mtazamo huo, wakiamini maisha sasa yamebadilika, ile dhana ya mtoto wa mwisho kudekezwa na wa kwanza kuwa kiongozi haipo tena kama ilivyo kwa Faraja Joseph anayesema siku hizi hakuna tofauti ya mzaliwa wa kwanza wala wa mwisho, mazingira ndiyo yatakulazimisha uishi vipi.
“Maisha ya zamani ndiyo yaliwatengeneza wazaliwa wa kwanza kuwa viongozi na wale wa mwisho kudekezwa, lakini sio sasa hivi. Ukiwa wa mwisho halafu uishi kwa kudeka, ‘hutoboi’ ukubwani,” anasema.
Mtazamo wake ni tofauti na wa Chiando Masatu ambaye ni mzaliwa wa kwanza kwenye familia ya watoto tisa.
Yeye anaamini kuwa mzaliwa wa kwanza moja kwa moja unakuwa ni kiongozi na mbeba maono wa familia, ikitokea umeharibu, ni doa kwa familia nzima.
“Mfano ni mimi, tukiwa bado kwa wazazi, nilikuwa na jukumu la kuwahudumia wadogo zangu pale wazazi wanapokosekana nyumbani. Hata baada ya kuanza kujitegemea, jukumu hilo liliendelea kwa kuletewa wadogo zangu watatu niwalee na kuwasomesha,” anaeleza.
Naye Zawadi Makore ambaye ni mzaliwa wa kwanza anaeleza namna alivyopata shida na mumewe, Elvis ambaye ni mzaliwa wa mwisho.
“Nilikuwa nikimuona Elvis kama anachukulia mambo kirahisi, hajali vitu vya msingi, mama yangu ambaye sasa ni marehemu aliniambia nimzoee kwani mume wangu ni mtoto wa mwisho, hivi sasa tuna miaka sita ya ndoa, tunaelewana,” anasema Zawadi huku akitabasamu.
Akiuelezea mtazamo huo kwa muktadha wa saikolojia, Bwaya ambaye pia ni mwanasaikolojia, anasema mtoto wa kwanza mara nyingi huzaliwa na wazazi vijana ambao ndio kwanza wanaanza maisha, hivyo hutoa muda wao mwingi kwa ajili ya mtoto kuliko inavyokuwa kwa mtoto wa mwisho.
“Mtoto wa kwanza huwa karibu sana na wazazi na hivyo humfanya awe mtulivu kwa tabia na uhusiano wake na anapoendelea kukua, huwa anakabiliana na shinikizo kwenye familia na hana mtu mwingine wa kumtegemea,’’ anasema na kuongeza:
“Mara nyingi hujitambua mapema akifanya wajibu wake kwa familia na hilo hutokea kwa familia nyingi, anapozaliwa mdogo wake wazazi wengi huchukulia yule wa kwanza amekua mkubwa na hivyo wanamsikiliza zaidi huyu mdogo, hali hiyo ndiyo inayomfanya mtoto wa kwanza awe na ugomvi usioisha na mdogo wake maana muda wote huhisi anapendelewa, anasikilizwa kuliko yeye.”
Anasema inahitajika hekima kubwa kwa wazazi wanaposhughulikia malalamiko ya watoto na kutopuuza madai ya mtoto wa kwanza, kwa kufikiri ameshakua wakiamini hata asiposikilizwa haimuathiri.
Bwaya anasema mtoto wa mwisho huzaliwa kipindi ambacho wazazi wengi ni watu wazima, hivyo kama mzazi alikuwa mkali kwa watoto anakuwa ameshaona madhara na anajutia.
Anasema wazazi wengi huona malezi ya mtoto wa mwisho ndiyo nafasi ya kurekebisha makosa, wengi wao kuwalea kwa kuwadekeza kama yai lisilopaswa kuguswa.
Mwanasaikolojia mwingine, Deogratius Sukambi anasema mara nyingi mfumo wa malezi ya mzaliwa wa kwanza na mzaliwa wa mwisho ndiyo chanzo kwani huwa ni tofauti.
“Hii inatokana na sababu kadhaa ikiwamo uzoefu, mtoto wa kwanza anapokuja mambo mengi wazazi huwa hawayafahamu, wengine wanalea kwa hofu, kutokana na hofu hiyo wapo ambao watampuuza huyo mtoto na wengine kumdekeza,” anasema.
Anasema lipo kundi la watoto wa kwanza, ambao hulazimika kujilea kwa kuwa wazazi wao huwa hawajui wafanye nini.
“Wazaliwa wa kwanza wanapopata wadogo zao, wengi hujikuta kama ndiyo wazazi wasaidizi, watawalisha chakula wadogo zao, kuwaongoza shuleni na mambo mengine, hali inayosababisha wazaliwa wengi wa kwanza kuwa na haiba ya uongozi kwa kuhakikisha vitu vingi vinakwenda sawa,” anasema.
Kuhusu wazaliwa wa mwisho, anasema vitu vingi husisimamiwa na kundi la watu, hivyo wengi wao huamini maisha yamepangiliwa.
“Ukiwaweka katika mazingira fulani na kuwambia Wapangilie maisha, wengi wao huwa hawawezi,” anasema Sukambi.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema watoto wote ni sawa, japo katika Uislamu, mzaliwa wa kwanza wa kiume huwa na nafasi ya baba.
‘Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie) anasema mkubwa kuzaliwa katika ndugu huwa na nafasi ya baba, ni mlezi kwa wenzake na hata ikitokea baba akatangulia mbele ya haki, yeye huchukua nafasi hiyo kama mlezi,” anasema.
Kwa upande wake, Askofu msaidizi mstaafu wa Kanisa Katoliki, Methodius Kilaini, anasisitiza usawa kwa watoto wote, akibainisha kwamba mzaliwa wa kwanza kwenye familia nyingi huwa ni mtoto wa mfano na hupewa jukumu la kuwasimamia wadogo zake.
“Mtoto wa mwisho pia hapaswi kudekezwa,” anasema Askofu Kilaini akitania kwamba wazaliwa wengi wa kwanza pamoja na kuwa viongozi, wengi wao huwa hawana akili sana kulinganisha na wadogo zao.