Dar es Salaam. Katika dunia inayobadilika kwa kasi, jukumu la kukuza maadili kwa mtoto ni la pamoja. Wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.
Wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wanakua na msingi thabiti wa kimaadili. Maadili haya yatakuwa dira ya kuwasaidia kupambana na changamoto za kimaisha, kufanya uamuzi sahihi na kuchangia katika ujenzi wa taifa lenye mshikamano, haki na amani.
Bila kuwekeza katika maadili ya watoto wetu leo, kesho tutashuhudia jamii yenye misingi dhaifu na yenye changamoto kubwa za kimaadili.
Hivyo basi, malezi ya kimaadili si chaguo, bali ni wajibu wa kizazi cha sasa kwa ajili ya kizazi kijacho.
Nasema hivyo kwa sababu enzi ya sasa ambayo dunia inabadilika kwa kasi kubwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, mitindo ya maisha na mawasiliano ya kidijitali, changamoto ya kulea mtoto mwenye maadili imekuwa kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanakabiliana na jukumu zito la kuhakikisha watoto wanakua wakiwa na msingi imara wa maadili unaowawezesha kutofautisha mema na mabaya.
Maadili haya si tu yanasaidia katika malezi binafsi ya mtoto, bali pia ni msingi wa ujenzi wa taifa lenye mshikamano na amani. Geofrey Swai mtaalamu wa malezi anasema maadili ni kanuni na mwongozo unaomsaidia mtu kuishi maisha yenye nidhamu, heshima na uwajibikaji.
Hivyo, anasema kwa mtoto, maadili yanakuwa dira ya kumsaidia kufanya uamuzi sahihi hata anapokuwa peke yake.
Swai anasema maadili kama vile ukweli, uaminifu, upendo, heshima kwa watu wengine, na uvumilivu, humsaidia mtoto kuwa na tabia bora zinazojenga uhusiano mzuri na watu anaoishi nao.
Anasema bila maadili, mtoto anaweza kukua akiwa na mtazamo wa kujitafutia manufaa binafsi tu, jambo linaloweza kuchochea mmomonyoko wa maadili au hata ule ushirikiano na jamii inayomzunguka.
Alisema Swai kwa nyakati hizo tulizo nazo liko wazi. Licha ya kuyaangalia mabadiliko ya kidijitali na kimaendeleo yanayoleta faida kubwa, lakini pia yameongeza changamoto kwa wazazi na watoto wenyewe.
Mtoto wa leo anapata taarifa nyingi kupitia mitandao ya kijamii, michezo ya mtandaoni na vyombo vya habari kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Mara nyingi taarifa hizi hubeba mafunzo yenye manufaa, lakini wakati mwingine hueneza tabia zisizofaa au mitazamo inayoweza kupotosha. Hali hii humweka mtoto katika mazingira magumu ya kuchagua kati ya maadili sahihi na vishawishi vinavyopingana na misingi ya familia na ya jamii.
Kukabiliana na hili, wazazi na walezi wanayo nafasi ya kwanza na ya moja kwa moja katika kukuza maadili ya mtoto.
Na mara zote malezi huanzia nyumbani na mtoto hufundishwa kwa matendo zaidi kuliko maneno. Wazazi wanapokuwa na nidhamu, ukweli, heshima na mshikamano, huiga moja kwa moja.
Hivyo basi, mzazi anapomwambia mtoto asiseme uongo huku yeye mwenyewe anaonekana akifanya hivyo, ujumbe unaotumwa kwa mtoto huwa na mkanganyiko. Hali hii huonesha kwamba wazazi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kutokana na tabia zao.
Dini ni nguzo kuu katika malezi ya kimaadili kwa tangu enzi ya mababu zetu. Na dini ni darasa tosha la mtoto kujifunza kuwa na hofu ya Mungu, kujifunza kuwa na upendo kwa jirani na kujiepusha na maovu. Kumpa mtoto malezi ya kidini kunamjenga kisaikolojia na kiroho, kumfanya awe na uthabiti wa kupinga majaribu ya maadili potofu.
Hata hivyo, wazazi wanapaswa kuzingatia kuwa ni muhimu dini ifundishwe kwa njia inayomfanya mtoto aelewe maana halisi ya mafunzo hayo badala ya kushurutishwa kuyafuata bila kuelewa.
Nasema hivyo kwa sababu watoo wengi hivi sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kimaadili kutokana na mitandao ya kijamii inayosambaza maudhui yasiyofaa.
Mabadiliko ya mfumo wa familia kama vile ongezeko la familia za mzazi mmoja na upungufu wa muda wa kulea kutokana na majukumu ya kiuchumi, yamechangia pia kupunguza umakini wa malezi ya kimaadili.
Hali hii inawaweka watoto kwenye nafasi hatarishi ya kujifunza tabia zisizofaa kutoka nje ya familia.
Ili kukabiliana na hili, ni muhimu kuwajengea watoto misingi ya maadili wakiwa wadogo. Misingi ya maadili inapojengeka mapema kwa mtoto, ni rahisi sana kuendelea nayo kadiri wanavyokua.
Lakini pia kutumia mazungumzo ya wazi na watoto kuhusu changamoto wanazokutana nazo kunawasaidia kutofautisha mema na mabaya. Jamii pia inapaswa kushirikiana katika kuhakikisha maadili yanafundishwa na kuendelezwa kwa njia mbalimbali.
Yupo mtaalamu mmoja niliwahi kuzungumza naye, aliniambia kuwa wazazi nao wanapaswa kutumia teknolojia kwa faida ya malezi.
Badala ya kuikataa mitandao ya kijamii, wazazi wanaweza kusimamia matumizi yake na kuhakikisha watoto wanapata elimu sahihi kupitia nyenzo hizo.
Programu za elimu, video zenye mafunzo na mijadala ya kimaadili zinaweza kutumika pia kuimarisha tabia bora za watoto.