Mbuni yaandika rekodi mpya Championship

BAADA ya Mbuni kuanza vyema Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, kwa kuifunga Mbeya Kwanza mabao 4-0, Oktoba 10, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, timu hiyo imeweka rekodi mpya tangu ianze kushiriki mashindano hayo.

Mabao ya Laurent Mloge, Frank Rutha, Rishedi Kihedu na Astidi Makomo, yameifanya timu hiyo kuandika rekodi mbili mpya na ya kwanza ni ya kushinda mfululizo dhidi ya kikosi cha Mbeya Kwanza, huku ya pili ni ya idadi kubwa ya mabao.

Iko hivi, tangu Mbuni aanze kucheze Ligi ya Championship msimu wa 2022-2023, mechi ya Oktoba 10, ilikuwa ni ya saba kukutana na Mbeya Kwanza na ushindi huo ni wa pili tena mfululizo na kwa idadi kubwa ya mabao, huku mitano iliyobaki ikichapwa.

Msimu wa 2022-2023, Mbuni ilichapwa bao 1-0, Novemba 12, 2022, ikachapwa tena raundi ya pili mabao 2-1, Machi 25, 2023, kisha msimu wa 2023-2024, ikafungwa 2-1, Oktoba 21, 2023, huku mzunguko wa pili ikapoteza pia 2-1, Februari 16, 2024.

Kwa msimu wa 2024-2025, ilianza kuchapwa mabao 2-1, mechi ya raundi ya kwanza, Januari 10, 2025, huku mzunguko wa pili ikashinda 3-2, Mei 11, 2025, kisha msimu huu wa 2025-2026, ikaendeleza tena ubabe pia kwa kushinda 4-0, Oktoba 10, 2025.