OKTOBA 10, 2025, Pacome Zouzoua alikiwasha kwa dakika 90 katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 akiitumikia Ivory Coast wakati ikiichapa Shelisheli mabao 0-7 ugenini kwenye Uwanja wa National Sports Complex nchini Mauritius, ikiwa ni mechi ya Kundi F.
Pacome alianza kikosini huku mastaa wengine wakiishia benchi mazima kama Amad Diallo wa Manchester United ya Ligi Kuu England na Nicolas Pépé (Villarreal, Hispania), huku Simon Adingra anayeitumikia Sunderland ya Ligi Kuu England akitokea benchi.
Kwa namna Pacome alivyopenya kikosi cha kwanza na kucheza dakika zote tisini ikiwa ni mara yake ya kwanza kuitwa na kucheza, imewafanya baadhi ya makocha kuona Yanga inapaswa kujipanga kwa lolote kutokana na nafasi hiyo aliyoipata.
Hata hivyo, Pacome ambaye Julai 2025 alisaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga hadi mwaka 2027, kama kuna timu itamuhitaji kwa sasa, inapaswa kwenda mezani kuuvunja, hivyo itakuwa faida kwa Yanga kumuuza kama ilivyokuwa kwa Stephane Aziz KI aliyesajiliwa na Wydad Casablanca ya Morocco, wakati msimu wa 2024-2025 ukielekea ukingoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi ambaye wakati Pacome anatua alielekea AS FAR Rabat ya Morocco kisha Kaizer Chiefs aliyoaga hivi karibuni, amesema, kiungo huyo ni mchezaji ambaye ameonyesha daraja lake la ubora ni kubwa, huku akibainisha kucheza mechi kama ile tena akiwa na wachezaji wanaocheza klabu tofauti za Ulaya, sio jambo la kawaida.
Amesema Pacome ni mchezaji ambaye ubora wake utamfungulia milango ya kwenda hata kucheza Ulaya, akifichua ni bahati sana kwa Yanga kuwa na mchezaji mwenye daraja kubwa.
“Kiwango chake kitaipandisha Yanga, pia Ligi ya Tanzania, kwani ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kucheza kiwango kikubwa kama kile.
“Pacome hii ni mara yake ya pili anaitwa katika kikosi cha Ivory Coast, lakini kocha amemuamini na kumpa nafasi kuanza kikosi cha kwanza akicheza dakika zote tisini, hii ni ishara kwamba tayari ameshaanza kuaminika na kwa muda aliocheza Yanga ijipange na ofa tu,” amesema Nabi aliyeipeleka Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.
Kocha Julie Chevalier aliyemfundisha Pacome kwenye kikosi cha ASEC Mimosas, alisema dakika 90 za Pacome zimeonyesha ni mchezaji ambaye yuko fiti sana na ana juhudi kubwa za mazoezi.
“Kwa wachezaji raia wa Ivory Coast wanaocheza Afrika, Pacome ndiye mtu anayefuatiliwa na wengi na wengi wamefurahi kuona anapata nafasi.
“Kiwango alichoonyesha sio kitu rahisi kwani ataifanyia mapinduzi timu ya taifa kutokana na ubora wake kwa kuingia tena kwenye mechi zijazo,” amesema.
Pacome katika mechi hiyo licha ya kutofunga wala kutoa pasi ya bao, alihusika kwenye tukio la penalti iliyoipata Ivory Coast dakika ya sita kwani pasi yake ya mwisho kwenda kwa Evann Guessand, mchezaji huyo aliangushwa eneo la hatari, ndipo Ibrahim Sangaré akafunga bao la kwanza.
Kwa mara ya kwanza, Pacome alijumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 53 kilichoandaliwa kwa ajili ya AFCON 2023 lakini baadae jina lake likatolewa baada ya mchujo kufanyika.
Mara ya pili kiungo huyo kujumuishwa kwenye kikosi hicho ilikuwa 2024, Ivory Coast ilialikwa kushiriki michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uruguay na Benin, Machi 2024 na kutokana na majeraha aliyokuwa nayo kipindi hicho, akashindwa kucheza.
Huu ukiwa ni msimu wa tatu Pacome anaitumikia Yanga baada ya kujiunga nayo Julai 2023 akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, kiungo huyo amekuwa na rekodi nzuri ya mchango wa mabao kikosini hapo.
Msimu wa kwanza 2023-2024 kwenye Ligi Kuu Bara, Pacome alihusika na mabao 11, akifunga saba na asisti nne. Kisha 2024-2025, akahusika na mabao 22, akifunga 12 na asisti 10. Msimu huu, 2025-2026, bado hajafunga lakini ana asisti moja, huku akiwa tayari ameisaidia kubeba Ngao ya Jamii akifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba.