TMA YAWAPIGA MSASA WATANGAZAJI WA AZAM MEDIA

……………………

Dar es Salaam:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa nchini (NMTC) imeendesha mafunzo maalum ya wiki mbili kwa watangazaji wa Azam Media kwa lengo la kuboresha uwasilishaji wa taarifa za hali ya hewa kwa umma kupitia chombo hicho cha habari. Mafunzo hayo, ambayo ni sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya TMA na Azam Media, yamefanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 10 Oktoba 2025.Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na kufungwa rasmi na Mkuu wa NMTC.

Akifungua rasmi mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, aliwataka watangazaji wa Azam Media kuwa miongoni mwa wataalamu bora barani Afrika katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

“Natarajia kuwa baada ya mafunzo haya, watangazaji wa Azam Media mtakuwa bora zaidi na kuwa mfano wa kuigwa katika Afrika, katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa ufanisi na weledi mkubwa” alisema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika uwasilishaji wa taarifa za hali ya hewa, akitoa wito kwa watangazaji kutumia mbinu mbalimbali za uwasilishaji ili kuvutia jamii na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya kila siku ya wananchi. 

Aliongeza kuwa TMA iko tayari kutoa mafunzo ya kina kuhusu utabiri wa hali ya hewa, jinsi ya kusoma dondoo muhimu za utabiri, na kuwawezesha watangazaji kuwa na uelewa wa kitaalamu wa sayansi ya hali ya hewa kulingana na majukumu yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari na Matukio wa Azam Media, Bi. Jane Shirima, aliishukuru TMA kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo na kuandaa programu hiyo. Alieleza kuwa mafunzo haya yanafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya Azam Media na TMA, ambapo awamu ya kwanza ilifanyika mwaka 2016 na awamu ya pili mwaka 2019.

“Mafunzo haya yatasaidia kuongeza ari, ufanisi na ubunifu katika uwasilishaji wa taarifa za hali ya hewa. Tunawashukuru TMA kwa kutupatia mafunzo haya muhimu kwa wakati muafaka,” alisema Bi. Shirima.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa, Bw. Peter Nick Mlonganile, alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia watangazaji kuwa wawakilishi na mabalozi bora kwa vyombo vya habari vingine kufika TMA na kupata mafunzo ya kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa umahiri.

“Elimu waliyoipata wanahabari wetu itawawezesha kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kuelimisha umma kuhusu hali ya hewa” alisema Bw. Mlonganile.

Warsha hii ni sehemu ya juhudi za TMA katika kuhakikisha kwamba taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa usahihi, kwa wakati na kwa njia rahisi, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu na dunia kwa ujumla zinakabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa