WHO: Watu milioni 150 Afrika wana matatizo ya afya ya akili

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, limesema takriban watu milioni 150 barani Afrika wanaishi na matatizo ya afya ya akili huku wengi wao wakikosa huduma muhimu za matibabu na ushauri nasaha.

Taarifa iliyotolewa Oktoba 10, 2025 na WHO imeeleza kuwa matatizo hayo yanachangiwa zaidi na msongo wa mawazo, wasiwasi uliopitiliza, pamoja na matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

WHO imeeleza kuwa changamoto kubwa inayokwamisha mapambano dhidi ya matatizo ya afya ya akili ni ukosefu wa rasilimali za kutosha, hususan bajeti ndogo zinazotengwa na serikali nyingi za Afrika katika sekta hiyo.

“Licha ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya akili, bado nchi nyingi hazijatoa kipaumbele kinachostahili katika mipango na bajeti zao,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa tatizo la watu kujiua kutokana na changamoto za afya ya akili limefikia wastani wa vifo 11.5 kwa kila watu 100,000, huku matumizi ya pombe yakionekana kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya bara hilo.

WHO imetoa wito kwa serikali za Afrika kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya akili, ikiwemo kuongeza idadi ya wataalamu wa saikolojia, kuimarisha vituo vya tiba, na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutambua na kukabiliana na changamoto za kiakili.

Kwa mujibu wa WHO, huduma bora za afya ya akili ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye ustawi, ubunifu na tija katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Endelea kufuatilia Mwananchi.