Askari Polisi auawa Arusha akidhaniwa mwizi

Arusha. Askari Polisi, Omary Mnandi (30), mkazi wa Jiji la Arusha, ameuawa usiku wa Oktoba 11, 2025 baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani akidhaniwa kuwa ni mwizi.

Tukio hilo lililotokea saa tano usiku katika baa iitwayo Simaloi iliyopo maeneo ya Kaloleni, jijini Arusha, tayari watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya Mnandi (marehemu) kuingia kwenye gari lingine badala ya gari lake, hivyo kudhaniwa kuwa ni mwizi.

Amesema kuwa baada ya Mnandi kuingia na kulala ndani ya gari hilo, watuhumiwa hao walimkuta na kuanza kumshambulia hadi umauti ulipomkuta.

“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za mauaji hayo, na uchunguzi wa tukio hili unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuatwe,” amesema.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa taratibu za mazishi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, marehemu Mnandi alikuwa na wenzake wakijiburudisha kwa vinywaji vya pombe katika baa hiyo kabla ya mauti kumkuta.

Richard Levina, amesema kuwa marehemu akiwa na askari wenzake wawili walifika katika baa hiyo mapema na kuanza kupata vinywaji vyenye kilevi.

Amesema ilipofika saa tano usiku, Mnandi alizidiwa na kilevi na kuaga wenzake kwenda kupumzika ndani ya gari lake.

“Hata hivyo, kwa bahati mbaya, alifungua na kuingia katika gari lingine lililokuwa jirani, akidhani ni lake, bila kujua kuwa si lake,” amesema.

Levina amesema kuwa baada ya kuingia, alilala usingizi mzito ndani ya gari hilo kabla ya wamiliki kurejea na kushangazwa kumkuta mtu wasiyemjua akiwa amelala ndani.

“Katika hali ya taharuki, walimshambulia kwa kipande cha chuma wakidhani ni jambazi, na kumsababishia majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake papo hapo,” amesema.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa marehemu Mnandi alikuwa akiishi katika nyumba za askari polisi (line polisi) eneo la Fire, jijini Arusha, na anatarajiwa kusafirishwa kwa mazishi mkoani Tanga leo, Oktoba 12, 2025.