::::::::::::::
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia ACT-Wazalendo, Bi. Rahma Mwita, amewaomba wakazi wa Kata ya Makumbusho kuwachagua viongozi wa chama hicho ili kuondoa kabisa tatizo la maji ya chumvi katika maeneo yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni, Bi. Rahma alisema kina mama wengi wamekuwa wakihangaika kwa miaka mingi kupata maji safi na salama, jambo ambalo ni kero na hatari kwa afya ya familia.
Alieleza kuwa yeye na Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Ramadhani Mzee, wamejipanga kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka pindi wakipewa ridhaa na wananchi.
“ACT-Wazalendo tunakuja na suluhisho la kweli. Tupewe nafasi, tutakomesha mateso haya ya maji ya chumvi,” alisisitiza huku akipigiwa makofi na wananchi waliokuwa na hamasa kubwa.