Santos aanza mazoezi ya viungo baada ya kupona

KINDA wa Kitanzania anayekipiga katika klabu ya Ceu Ciutat Meridiana ya Hispania, Fahmar Santos ameanza mazoezi mepesi ya viungo ikiwa ni sehemu ya kurejea uwanjani baada ya jeraha la goti.

Santos (21) alipata jeraha hilo mwishoni mwa msimu uliopita na kulazimika kufanyiwa operesheni Agosti 8 mwaka huu, jambo lililomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Kwa sasa, kinda huyo ameanza hatua ya awali ya kurejesha uimara wa mguu wake kupitia mazoezi mepesi ya viungo chini ya usimamizi wa wataalamu wa tiba ya michezo wa timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti Santos amesema anaendelea vizuri na ripoti zinaeleza atarejea rasmi uwanjani Januari mwakani.

“Napiga hatua nzuri kwa sasa naendelea na mazoezi ya viungo madogo madogo. Timu ya matibabu imeridhishwa na maendeleo yangu na matumaini ni makubwa, kuna ofa zilitokea lakini changamoto ilinikuta baada ya kupata majeraha.”

Fahmar ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa vijana wenye kipaji kikubwa kutoka Tanzania amekuwa akitazamwa kama mmoja wa wachezaji watakaokuwa mfano kwa chipukizi wengine wanaotamani kufika mbali kupitia soka.

Kiungo huyo alijiunga na timu hiyo msimu wa 2022/23 akitokea Ruvu Shooting aliyoitumikia kwa misimu miwili 2019/20 na 2020/21 na Zanzibar alicheza katika akademi ya Deal Kids.