Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema Serikali atakayoiunda itazipa kipaumbele bidhaa zote zinazozalishwa visiwani humo ili kushindana katika soko la kimataifa.
Amesema bidhaa hizo ni pamoja na zile zinazotokana na useremala na kazi za mikono, na atahakikisha anawashika mkono wanaojishughulisha na shughuli hizo ili kuinua uchumi wa wananchi wa Zanzibar.
Othman ameeleza hayo leo Jumapili, Oktoba 2025, alipowatembelea wajasiriamali, wauzaji na watengenezaji wa fenicha wa eneo la Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mwendelezo wa kampeni za kusaka kura, akikutana na makundi mbalimbali kabla ya kufanya mkutano wa hadhara.
Katika maelezo yake, Othman amesema kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikitambulika kwa uzalishaji wa bidhaa bora, zenye ubunifu wa kipekee ulionakishiwa kwa michoro ya kuvutia, lakini mifumo iliyopo na ukosefu wa masoko umewafanya mafundi hao kubaki katika umaskini.

Mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya ACT Wazalendo Othman Masoud Othman akikagua fenicha mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali wa Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja alipowatembelea wazalishaji hao kwa lengo kusikiliza kero zinazowakabili
Pia, Othman amesema Zanzibar imekuwa ikitajwa tangu zama za zamani kwa useremala na ubunifu wa mikono, lakini sasa mafundi wengi wako kwenye ugumu wa maisha kutokana na kukosekana kwa sera bora za uendelezaji wa sekta hiyo.
“Niwaahidi, Serikali ya ACT – Wazalendo itahakikisha wajasiriamali wadogo wanapatiwa mikopo nafuu, elimu ya biashara pamoja na fursa za mafunzo ya kisasa ili bidhaa zao ziingie katika viwango vya kimataifa,” amesema na kuongeza:
“Tutaweka utaratibu wa masoko ya kimataifa ya bidhaa za asili za Zanzibar kama vile samani, vinyago, bidhaa za mwani, viungo na nguo zenye vionjo vya utamaduni wa Kizanzibari, ili kuimarisha uchumi wa wananchi wa kisiwa hiki.”
Othman amesema Zanzibar ni kisiwa chenye utajiri wa ubunifu na bidhaa za kipekee zinazoweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, wanawake na mafundi wa ndani, lakini hilo litafanikiwa endapo kutawekewa utaratibu wa kutangazwa na kuwekewa sera madhubuti.
Mgombea huyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Wazanzibari kuwa na dhamira ya kweli ya mabadiliko Oktoba 29 kwa kumchagua awe Rais ili kuendeleza rasilimali zao na kuzitumia kwa manufaa ya watu wote.
“Mnapaswa kuchagua kwa matumaini, si kwa mazoea. Serikali ya ACT – Wazalendo itahakikisha kila bidhaa inayozalishwa Zanzibar inapewa thamani na kufikishwa katika soko la kimataifa,” ameeleza.
Katibu wa Mkokotoni Fenicha, Othman Ali Othman, amemweleza Othman kuwa wajasiriamali wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa soko la bidhaa zao licha ya kuzizalisha katika hali ya ubora unaotakiwa.
“Changamoto nyingine, eneo tunalofanyia kazi ni dogo, kwa sababu tuna uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingi zaidi ya hizi. Tunaomba ukiingia madarakani ututafutie eneo jingine ili kuboresha shughuli zetu,” amesema Othman.
Kabla ya kuzungumza na wajasiriamali hao, Othman alifanya mkutano na wauza dagaa wa Fungu Refu, mkoani humo, ambapo amewaahidi kushughulikia changamoto ya ukosefu wa masoko, miundombinu duni na vikwazo katika utoaji wa leseni.
Othman, ambaye ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa ataweka mazingira bora zaidi katika shughuli zao ili wajikwamue kiuchumi.
“Serikali ninayotarajia kuunda itatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo ili kuchangia ipasavyo kukuza uchumi wa Zanzibar. Wafanyabiashara wadogo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, tukiwapa nguvu na haki, tutakuwa tumewainua wananchi wote,” amesema.