Kibonde: Kila Mtanzania atapanda ndege

Dar es Salaam. Kupanda ndege imekuwa ni ndoto ya kila mtoto. Hata hivyo, baadhi yao wanakuwa watu wazima bila kupanda usafiri huo kutokana na changamoto za kipato kitakachowawezesha kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kwa haraka.

Mgombea urais wa Demokrasia Makini (Makini), Coaster Kibonde ameahidi kutimiza ndoto ya Watanzania wengi kwa kufanya usafiri wa ndege kuwa wa kawaida, utakaotumiwa na kila mtu kwa ajili ya kusafiri au kusafirisha mizigo.

Kibonde na wagombea wengine 16 wa vyama vya siasa, wanazunguka nchi nzima kuomba kura kwa wananchi huku wakitoa ahadi na kunadi ilani za vyama vyao kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 12, 2025 akiwa Butiama mkoani Mara, Kibonde amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha kila mwananchi anatumia usafiri wa ndege.

Amesema atahakikisha ananunua ndege 70 aina ya Bombadier na kwamba kila mkoa nchini unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa ili mtu aweze kwenda popote atakapo kwa kutumia usafiri huo kwa gharama nafuu.

“Tunataka kila mkoa kuwe na kiwanja cha ndege ambacho ndege zitatua saa 24 na viwanja vikubwa ambavyo ndege kubwa za mizigo, ndege kubwa za abiria zitatua. Hii yote ni kuwavuta wanaokuja kununua malighafi mbalimbali nchini kufika kwenye mkoa husika,” amesema.

Mgombea huyo amesema amelenga usafiri wa Bombadier kwa sababu ni usafiri mzuri ambao unaweza kwenda maeneo yote kulingana na hali ya hewa ya Tanzania na hali ya viwanja vilivyopo sasa.

Kuhusu uwezo wa kununua ndege hizo, Kibonde amewatoa shaka Watanzania kwamba biashara ya ndege siyo lazima kutoa fedha taslimu, bali serikali yake itazungumza na kampuni zinazotengeneza ndege ili wawapatie hizo ndege na itawalipa kadiri wanavyotoa huduma.

“Tunakwenda kuliinua shirika la ndege la Air Tanzania, liwe na ndege za kutosha na Watanzania waweze kupanda, tukiamini kwamba Watanzania wengi huwa hawatumii ndege, bali magari na treni na meli kwa upande wa majini.

“Kwa mara ya kwanza, tunahitaji Watanzania watumie ndege nchini kwao. Ndiyo maana nimesema ili kila Mtanzania aweze kupanda ndege, serikali yangu itashusha bei ya tiketi ili Watanzania, wakulima wa hali ya chini wapande ndege mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya,” amesisitiza Kibonde.

Mgombea huyo amesisitiza kwamba hilo likifanikiwa, Tanzania inakwenda kukua kiuchumi kuanzia uchumi wa mwananchi mmojammoja hadi uchumi wa Taifa kwa sababu usafiri huo utafungamanishwa na shughuli zao.

Amebainisha kwamba hali ya sasa ya uendeshaji wa shirika la ndege, serikali iliyopo madarakani imejitahidi kwa kiasi fulani, lakini wao Makini bado hawajaridhika ndiyo maana wanataka kwenda kuboresha ili kuwa na ndege za kutosha na kushusha gharama zake.

Kibonde amebainisha kwamba wanakwenda kuboresha viwanja vya ndege kubwa na ndogo zitue usiku na mchana, pia, viwanja hivyo vitoe huduma bora kwa abiria kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Katika ndege hizo (Bombadier) 70, ndege tano zitakuwa za mizigo, kutoa mzigo kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine. Tunakwenda kuhamasisha kilimo cha mbogamboga, kwamba mboga zitoke Katavi, zifike kwa wakati Dar es Salaam,” amefafanua.

Akizungumzia usafiri wa treni ya kisasa, mgombea huyo amesema wakati ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ukiendelea kutoka Dodoma kwenda mikoa mingine ya Singida hadi Tabora na Kigoma, serikali yake itaanza ujenzi wa treni hiyo kutoka Morogoro kwenda Iringa – Mbeya – Rukwa – Katavi – Kigoma.

“Sisi tumesema, tutajenga SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Mbeya, kwa maana kwamba itapita Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya hadi Songwe. Kutakuwa na SGR nyingine itakwenda mpaka Sumbawanga na itaunganisha na nyingine inayotoka Mpanda – Kaliua (Tabora) – Kigoma,” amesema mgombea huyo.

Amesisitiza kwamba serikali ya makini ikiingia madarakani itahakikisha mkandarasi aliyepo kazini anakamilisha kazi hiyo haraka na wataanzisha ujenzi kwenye maeneo mapya ili Watanzania wote watumie usafiri huo.

Kibonde amebainisha kwamba maeneo yote yenye vivuko, Watanzania watavuka bure kwa kutumia vivuko hivyo nchi nzima isipokuwa kwa magari, pikipiki na baiskeli, ndizo zitakazolipiwa. Lengo la kuja na utaratibu huo ni kuwapunguzia mzigo wananchi ambao kila siku lazima wavuke kwenye shughuli zao.

“Tunakwenda kuimarisha meli katika Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na maziwa mengine. Tunakwenda kuziimarisha, kuziboresha na ikiwezekana kununua mpya kuhakikisha kwamba wote wanaotumia usafiri wa majini waneemeke na serikali ya Makini,” amesema.

Amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura Oktoba 29, 2025 na kumchagua yeye ili awe Rais wa saba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, amewataka wahifadhi amani na kuepuka maandamano yanayohamasishwa mitandaoni.

“Ninawaomba Watanzania wawapuuze wanaoandika mitandaoni kwamba Oktoba 29 ni maandamano. Hakuna maandamano Oktoba 29, ni siku ya kwenda kupiga kura,” amesisitiza mgombea huyo.