Arafat Masoud aanza na tatu Misri

KINDA wa ENNPI ya Ligi Kuu Misri, Arafat Masoud ‘Konde Boy’ amesema ameanza na mechi tatu za kirafiki akifunga bao moja na kutoa asisti mbili.

Kinda huyo alijiunga na Azam mwaka 2017 akicheza timu za vijana za U-17 na U-20 kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa, na msimu uliopita aliichezea Fountain Gate kwa mkopo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Konde Boy amesema baada ya kupata kibali cha kucheza ameanza kwa kiwango kizuri ambacho pia kimemkosha kocha wa timu hiyo, Sayed Yassin, ambaye amemsisitiza baadhi ya mambo ya kuyafanyia kazi.

Aliongeza kuwa ni hatua kubwa kucheza mechi hizo, ambazo anaamini kuwa kama akiendelea kufanya vizuri basi atapata nafasi ya kucheza hadi kwenye mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine makubwa.

“Nilikuwa nje ya uwanja kwa takribani mwezi nikisubiri mambo ya vibali, lakini sasa nimekamilisha kila kitu. Nilianza kucheza mechi za kirafiki moja dhidi ya timu kutoka Libya na nyingine ya hapa Misri,” amesema Konde Boy, na kuongeza:

“Kocha ameniambia mambo mengi, lakini ana imani kwamba nitaendelea kuonyesha kiwango kile cha kwenye mechi ya kirafiki. Na mimi nataka kuaminisha kuwa naweza, nimekuja kufanya kazi.”

Klabu ya nyota huyo iko nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imecheza mechi 10, ikishinda nne, sare tano na kupoteza moja, ikikusanya pointi 10.

Hadi sasa, wachezaji wa Kitanzania wanaokipiga kwenye ligi hiyo wako sita.