Nilisomea chini ya mti ila sababu ya elimu naishi vyema – Ole Millya

Mirerani. Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,  James Ole Millya ameiasa jamii ya wafugaji kusomesha watoto wao wakati huu wenye mazingira na miundombinu bora ya elimu kwani yeye alipata elimu ya msingi chini ya mti, kutokana na miundombinu duni iliyokuwapo wakati huo.

Hivi sasa miundombinu ya elimu na mazingira kwa jamii ya kifugaji imekuwa tofauti na miaka ya 1980 na 1990 kwani kulikuwa na shule chache tofauti na hivi sasa.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, James Ole Millya ameyasema hayo Oktoba 12 kwenye mahafali ya tano ya Shule ya Msingi Glisten iliyopo mji mdogo wa Mirerani.

Amesema hivi sasa mazingira ya miundombinu ya elimu ni bora tofauti na hivyo jamii ya wafugaji itumie fursa hiyo kwa kusomesha watoto wao.

“Mimi nimetoka kwenye familia duni nilipata elimu kwenye mazingira magumu ya kusoma chini ya mti ila nikapata ufadhili na sasa nina maisha mazuri sababu ya kupata elimu,” amesema Ole Millya.

Amesema alisomea chini ya mti na wakati mvua ikinyesha wanafunga shule ila akapambana hivyohivyo na sasa ana mafanikio makubwa kupitia elimu.

Amesema kupitia elimu amemjengea nyumba mama yake mzazi, amekuwa mbunge Simanjiro, Bunge la Afrika Mashariki na sasa anagombea ubunge kupitia CCM.

“Mwaka 2004 nilipata shahada yangu ya kwanza ya sheria nikiwa miongoni mwa watoto wa jamii ya kifugaji wa kwanza kwanza Simanjiro kutunukiwa hilo, kwa hiyo wazazi na walezi tusomeshe watoto,” amesema Ole Millya.

Ameeleza kuwa mgombea urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan alipofika mkoani Manyara alimuelezea suala la elimu lilivyo changamoto Simanjiro.

“Mgombea Samia amefanya mapinduzi makubwa ya elimu kwa kutoa fedha nyingi za miundombinu ila nilitoa ombi Simanjiro tujengewe shule za bweni, kwani bado kuna maeneo watoto wanatembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni,” amesema.

Mkurugenzi wa Shule ya Glisten, Justin Nyari ambaye ni mmiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite ameiasa jamii kushiriki uchaguzi mkuu kwa kujitokeza kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.

“Mimi nimewekeza kwenye elimu kwa ajili ya kusaidia jamii kupata elimu, tumeona sera nzuri za Serikali hivyo tuiunge mkono kwa kuchagua viongozi tunaowapenda Oktoba 29,” amesema Nyari

Mmoja kati ya wahitimu hao, Faraja Makeseni ameeleza kwamba anatarajia kufaulu na mwakani 2026 atajiunga kidato cha kwanza kuanza elimu ya sekondari.

Makeseni ameeleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha anakuwa daktari kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii pindi akihitimu taaluma hiyo.