NYOTA wa kimataifa, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr ya Wanawake ameendelea kuonyesha kiwango bora kwenye mechi nne za ligi, akiwa anaongoza hadi sasa kwenye msimamo wa wafungaji kwa mabao sita.
Ndiye Mtanzania pekee anayecheza Ligi ya Saudia, na ndani ya misimu mitatu akiitumikia klabu hiyo akitokea Dux Logroño ya Hispania, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho, akiipa ubingwa mara mbili.
Msimu wa kwanza Clara alifunga mabao 11 na kutoa asisti saba, akaisaidia timu hiyo kutetea taji. Msimu uliofuata alifunga mabao 21 na kutoa asisti saba, na tayari msimu huu amefikisha mabao sita kwenye mechi nne.
Amekuwa nyota tishio kwenye ligi hiyo, na ubora wake umefanya aendelee kuaminiwa kwenye kikosi hicho, ambacho pia upande wa wanaume kinachezewa na nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo.
Uwepo wake umeipa mafanikio makubwa timu hiyo, ambayo hadi sasa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote kwenye mechi nne na iko kileleni mwa msimamo wa ligi.
Akizungumzia kiwango chake amesema: “Nashukuru kuwa mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa timu, na nina furaha hadi sasa tupo kileleni. Naamini kwa kushirikiana na wenzangu tutafanya vizuri.”
Kwa sasa, ligi ya nchi hiyo imesimama kwa mwezi mmoja kupisha majukumu ya timu za taifa. Itaendelea Nov 06 kwenye dabi ya Al Nassr v Al Hilal.