DILI la kocha anayesakwa na Yanga, Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ bado halijamalizika weka akiba ya maneno ambapo kumeibuka makundi mawili ndani ya timu hiyo huku moja likifanya mawasiliano ya siri na kocha huyo.
Iko hivi, Roro amefanya mawasiliano na mabosi baadhi wa Yanga wakimpa kocha huyo siku tatu kuamua juu ya hatma yake juu ya muundo wa benchi lake la ufundi.
Kocha huyo anakuja kuchukua nafasi ya Romain Folz ambaye ameiongoza Yanga kuanzia mwanzoni mwa msimu huu, amecheza michezo mitano ya mashindano ameshinda minne, ametoka sare mmoja timu yake ikiwa imefunga mabao tisa bila kuruhusu bao lolote.
Hata hivyo, kumekuwa na mgawanyiko mkubwa kwa mashabiki, wengine wakitaka Folz abaki klabuni hapo kwa kuwa timu yake haijapoteza, lakini wengine wakitaka aondoke kwa kuwa timu haichezi vizuri.

Roro amekubali kubadili msaidizi wake tofauti na yule wa awali aliyempendekeza kuja naye ambaye Yanga imemkataa kwa kukosa sifa stahiki juu ya leseni yake ya ukocha.
Kulainika kwa Roro, kumeifanya Yanga kumpa presha ikimtaka kutumia siku tatu kuanzia leo kufanya uamuzi wa mwisho haraka juu ya kutafuta msaidizi mwingine.
Kama Roro atashindwa kufanya hivyo, mabosi wa Yanga wataondoa dili hilo mezani na kuamua kutembea na akili nyingine ambayo itakuwa kama imefuta nafasi ya kocha huyo raia wa Madagascar.
Mbali na hilo, Roro pia ametakiwa kukubaliana na kuendelea na kocha wa sasa wa mazoezi ya viungo Tshephang ‘Chyna’ Mokaila, raia wa Botswana, ambaye mabosi wa Yanga wanamuona bado ni mtu bora kwao.

“Kocha amekubali, sasa tusubiri kama atatekeleza. Anatakiwa ndani ya siku tatu awe ameshatuma jina jipya tofauti na hapo tutafanya uamuzi mwngine,” kilisema chanzo chetu.
“Hili la msaidizi anatakiwa kukabiliana nalo tu ingawa anaonekana kukubali kwa shingo upande, lakini huo ndio msimamo wetu, sasa tunasubiri wiki hii akituma mrejesho tutachukua hatua.”
Wakati msimamo wa mabosi wanaotaka kuletwa kwa kocha mpya ukiwa hivyo, kuna kundi lingine la mabosi limeibuka likisema halikubaliani na kubadilishwa kwa kocha wa sasa Romain Folz.
Msimamo wa kundi hili umetokana na mabadiliko ambayo Folz ameanza kuyaonyesha kwenye kikosi hicho, ikielezwa kwamba kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya TRA United uliochezwa juzi, licha ya kumalizika kwa sare isiyo na mabao lakini timu yao iliupiga mpira mwingi.

Mabosi hao wanaona kama watakuwa wanamuonea kocha huyo, wakipeleka presha kwamba kocha huyo apewe muda zaidi kabla ya kuchukua uamuzi huo mkubwa.
“Ungekuwa uwanjani kwenye mchezo wa TRA ungeona namna mambo yameanza kubadilika, utasema sio timu hii ambayo tunataka kubadilisha kocha, timu imecheza mpira mkubwa sana,” amesema bosi huyo.
“Hiyo kutoka sare ni matatizo ya wachezaji wenyewe tu, wamepoteza sana nafasi za kufunga, hapo kocha anakosa gani, kwahiyo utaona namna ni hoja ngumu kuingia akilini kwasasa kumtimua kocha.”

Wakati mabishano hayo ya hoja yakiendelea, yanamsubiri rais wa Yanga injinia Hersi Said ambaye alikuwa nje kikazi akitarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia jana, akitokea Italia alikokwenda kuhudhuria mkutano wa umoja wa klabu barani Ulaya (ECA).
Kurejea kwa Hersi, Mwanaspoti linafahamu atakutana na makamu wake Arafat Haji aliyekuwa nchini, kutoa hatma ya uamuzi kuhusu kocha huyo.