Samia aahidi soko la kisasa, maghala ya chakula Mbogwe

Mbogwe. Ujenzi wa soko la kisasa, maghala ya chakula na mradi wa maji utakaoondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa baadhi ya kata zinazokabiliwa na maji, ni miongoni mwa ahadi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ili kuchechemua biashara.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi hizo na nyingine zilizoainishwa kwenye ilani ya chama hicho, zitakazotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwapo watachaguliwa tena.

Samia ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 12, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni mkoani Geita, uliofanyika katika kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe baada ya jana kumaliza kampeni zake mkoani Shinyanga.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Masumbwe,wilayani Mbogwe mkoa wa Geita,waliojitokeza kusikiliza sera za mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan,leo Jumapili Oktoba 12,2025.

Samia amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza kwa kipindi kijacho, atashughulikia tatizo la upungufu wa maji katika baadhi ya kata zilizopo wilayani humo na kuhakikisha adha hiyo inaondoka.

Amesema hadi sasa asilimia 86 ya wananchi wilayani humo wanapata huduma ya maji safi na salama na kuwa akichaguliwa atahakikisha asilimia 14 iliyosalia wanapata huduma hiyo muhimu kupitia mradi wa maji wa Masumbwe kutoka Ziwa Victoria, unaoendelea kutekelezwa ambao kwa sasa umefikia asilimia 68 na utamaliza adha hiyo.

“Tumepiga hatua katika kufikisha huduma ya maji katika wilaya hii na tumefikisha asilimia 86, najua kuna kata ambazo zinakabiliwa na upungufu wa maji hususani kipindi hiki cha kiangazi ikiwemo kata ya Mbogwe, habari njema ni kwamba mradi wa maji wa thamani ya Sh4.3 bilioni utasaidia kumaliza tatizo hili na mradi umefikia asilimia 68,” amesema.

Pia, amesema ilani ya chama hicho ya mwaka 2025/30 imeahidi kujenga soko kubwa la kisasa wilayani humo, maghala ya chakula ili kutengeneza fursa kwa wakazi hao na kuchechemua biashara.

“Mbali na kuongeza bajeti ya Tarura, tutajenga barabara ya kuelekea makao makuu ya wilaya yenye urefu wa kilomita 45 ili kurahisisha shughuli za usafiri kwa manufaa ya wananchi wa maeneo hayo,” ameongeza.

Kuhusu madini, mgombea huyo amesema Serikali ilianzisha mkoa wa kimadini wilayani Mbogwe ili kufikisha huduma hiyo karibu na wachimbaji.

Amesema kwa kutambua na kujali mchango wa sekta ya madini, Serikali itafanya utafiti wa maeneo yenye madini ambapo mpaka sasa imepima asilimia 16 tu nchi nzima, na lengo ni kubaini maeneo mengine yenye madini na kipaumbele ni wachimbaji wadogo.

Sehemu ya Wananchi wa Bukombe mkoani Geita waliohudhuria mkutano wa Kampeni wa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ,Samia Suluhu Hassan, leo Jumapili Oktoba 12, 2025.

Kuhusu sekta ya afya, Samia amesema wamefanya maboresho katika Hospitali ya Wilaya na lengo la Serikali ni kila mwananchi apate huduma ya afya karibu na eneo lake.

Kuhusu sekta nyingine kama elimu, maji, umeme na miundombinu, amesema hiyo ni shughuli endelevu kwa sababu ni maendeleo ya jamii ambayo lazima yashughulikiwe kila wakati.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Anna Gabriel amesema maboresho ya sekta ya afya yamesaidia wanawake na watoto na kuwa kwa sasa hawafuati huduma za afya mbali na makazi yao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Awali, kina mama na watoto tulikiwa tunapata adha ya huduma ya afya, ila kwa sasa huduma hizo zimesogezwa kwenye maeneo yetu na hospitali za wilaya zimeboreshwa pia,” ameongeza.