Kauli za wananchi mwendokasi Mbagala ikitesti mitambo

Dar es Salaam. Baada ya kuanza kwa majaribio ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT) maarufu mwendokasi awamu ya pili Barabara ya Kilwa (Mbagala), madereva wa bajaji, pikipiki na daladala wamesema usafiri huo hautawaathiri huku abiria wakieleza matumaini pale utakapoanza rasmi.

Leo, Oktoba 12, 2025, madereva wa bajaji na bodaboda wameukaribisha usafiri huo wakisema baadhi yao wanaopakia abiria bila kukaa vituoni wataumia.

Wamesema neema pekee wanayoiona ni kwa wale wanaokaa kwenye vituo rasmi vya kupakia abiria, wakieleza kuwa kuanza kwa mradi huo ni neema ya kupata abiria wanaposhuka vituoni.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa ameiambia Mwananchi kuwa, majaribio ya usafiri huo yalianza tangu Oktoba 10  mwaka huu huku ya Leo, Oktoba 12, 2025 yakihusisha uwepo wa abiria ndani ya mabasi hayo.

Kuanza kwa majaribio hayo kunahitimisha mlolongo wa ahadi kuhusu lini mradi huo upande wa Mbagala ungeanza, baada ya danadana za muda mrefu.

Danadana hizo zimeonekana baada ya Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) Agosti 20, 2025 kutangaza kuwa, mabasi ya mwendokasi Barabara ya Kilwa yataanza safari Septemba mosi mwaka huu.

Ahadi hiyo haikutekelezeka kama ilivyoahidiwa kwa kuwa,  baadhi ya miundombinu haikukamilika hivyo siku rasmi ya kuanza huduma hiyo ikasogezwa hadi Septemba 15,2025.

Msemaji wa Serikali Msigwa amesema leo, Oktoba 12, 2025 kuwa, tayari majaribio yameanza.

“Majaribio yameanza tangu juzi (Ijumaa) na jana (Jumamosi) mabasi yalianza bila abiria, leo Jumapili (jana) yameanza kupakia abiria, tutakwenda hivi wakati tunaendelea kuongeza mabasi kwenye njia hiyo,” amesema.

Dereva bodaboda kutoka Mbagala Rashid Kachona amesema ujio wa usafiri huo hautawaathiri kwa kuwa, abiria wengi wanapenda kutumia usafiri huo.

“Abiria wa gari ni gari, kama ni bodaboda watatumia bodaboda, utakuta abiria yupo kwenye foleni lakini anasema hawezi kupanda bodaboda bora asubiri gari hilohilo.

“Kuanza kwa usafiri huu, kundi la bodaboda watakaoathirika ni wale wanaopandisha abiria wanapakia watu wawili kwa mkupuo kwa Sh2,000 kwa kila mtu, hao ndio hawatapata wateja, sisi tuliopo vituoni tunawasubiri abiria washuke kwenye hayo magari,” amesema bodaboda huyo.

Said Khamis dereva bodaboda Mbagala, amesema ana furaha kuona usafiri huo ukianza kwa majaribio kwa kuwa, kero ya usafiri Mbagala ni kubwa.

“Hatuoni kama mabasi haya yatatunyang’anya abiria ya yanakuja kuondoa changamoto ya usafiri,  kwa sababu abiria waliopo Mbagala ni wengi hata ujio wa mabasi haya changamoto bado haitaisha, tutashirikiana kuondoa changamoto ya usafiri,” amesema.

Pia, amesema bado wanaendelea kuwaelimisha madereva wenzao kutopita barabara inayotumiwa na mabasi hayo ili mradi huo ufanye kazi ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo, kwa kuwa wengi wanateseka kupata usafiri.

Mbagala ni kitovu muhimu cha usafiri kinachounganisha kata kadhaa ndani ya  Wilaya ya Temeke zikiwamo Mbagala kuu, Chamazi, Charambe, Toangoma, Mianzini, Kiburugwa na Kijichi.

Pia, ni kitovu kinachowaunganisha wakazi wa Msongola na wale wa maeneo ya mbali kama Zingiziwa na Chanika katika Wilaya ya Ilala, sambamba na wakazi wa Wilaya ya Mkuranga kutoka kata za Mwandege, Vikindu na Vianzi, mkoani Pwani.

Dereva bajaji, Shafii Mtiba amesema pamoja na hofu ya kupoteza abiria, zipo fursa watazipata kuanza kwa kazi kwa mabasi hayo.

 “Asubuhi huwa tunachukua watu wengi kuwapeleka mjini, kwa maana hiyo lazima kutakuwa na mabadiliko mradi huu ukianza, sasa tutaangalia njia zingine za ndani kuwapeleka abiria ili sote tufanye kazi ya kuwasaidia wananchi,” amesema.

Dereva wa daladala aliyejitambulisha kwa jina moja la Hans, amesema ujio wa mabasi hayo hautawaathiri kwa kuwa, bado daladala zinaendelea kuwepo barabarani.

“Sisi tutaendelea kuwepo, watatusaidia hawa kupunguza wingi wa abiria, Mbagala ina watu wengi, mabasi yanahitajika mengi zaidi sio tatizo la kutatuliwa ndani ya muda mfupi, kunahitajika muda wa kutosha,” amesema Hans.

Mfanyabishara wa eneo la Mbagala Rangi Tatu, Sharifa Yusuph amesema kuanza kwa mradi huo kutawapunguzia msongo wa mawazo wanaoupata kila wakiwaza usafiri.

“Ni hatua nzuri kuanza kwa mabasi hayo, kero yetu Mbagala ni usafiri; msongamano wa watu ni mkubwa na watu muda wote wanagombea daladala, tunapoongezewa usafiri huo, kwetu wametupunguzia mzigo,” amesema.

Lelya Shaban, mkazi wa Chanika akielezea ahueni yake kwa kuanza kwa usafiri huo, amesema utawaokolea muda wananchi pamoja na fedha nyingi wanazotumia kuwahi kwenye vibarua vyao.

“Mbagala usipoamka alfajiri sana, huwezi kuwahi unakokwenda kama unahitajika mapema, foleni ni kubwa sana na wakati mwingine gari linaweza kuharibika katikati ya safari msiwe na pakupita.

“Mwendokasi kwetu tunaona kama mkombozi utatusaidia sana, wamachinga, mama lishe na kina mama wanaowahi kununua samaki feri alfajiri,” amesema.

Mkazi wa Mwandege, Wilaya ya Mkuranga, Juma Abdul ambaye amepanda usafiri huo kwa majaribio alisema safari yake kutoka Mbagala hadi Gerezani leo ilikuwa ya kuvutia, lakini kuna changamoto za kiutendaji amezibaini.

“Nilisubiri takriban saa moja katika Kituo cha Mbagala Rangi Tatu kwa kuwa mabasi yaliyotolewa bado ni machache,” amesema.

Pia, Abdul amesema baadhi ya abiria walilazimika kusubiri kwa muda mrefu kwenye foleni kununua kadi za kielektroniki zinazotumika kuingia katika vituo vya BRT.

“Wengi wao walichelewa kununua kadi hizo kwa kuwa, uzinduzi wa huduma ulikuwa umeahirishwa mara kadhaa, hivyo walikuwa na shaka kama kweli ingetokea. Wengine walilazimika kuwalipa waliokuwa na kadi ili waweze kuingia,” amesema Abdul.

Hata hivyo, leo kwa kuwa huduma ni mpya, bajaji na pikipiki kadhaa zilionekana zikiendelea kutumia njia za BRT.