Shule ya Mashati kuunganishwa na nishati safi ya kupikia

Rombo. Wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, ameahidi kuiunganisha  Shule ya Sekondari   Mashati iliyopo wilayani Rombo, mfumo wa nishati safi ya kupikia.

Amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi za elimu, kwa lengo la kulinda misitu na kuboresha afya za watumiaji kupitia nishati mbadala isiyo na madhara kwa mazingira.

Profesa Silayo ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Oktoba 12, 2025, wakati wa mahafali ya 16 ya kidato cha nne yaliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo, jumla ya wanafunzi 138 wanatarajiwa kuhitimu masomo yao mwaka huu.

“Nimeelezwa kuwa shule hii haina mfumo wa nishati safi ya kupikia na kwa kuwa mimi ndiye mlezi wa shule hii, ni lazima tuhakikishe jiko la shule linakuwa na mfumo huo, kwa sababu sisi kama TFS tunahusika moja kwa moja na usimamizi wa rasilimali za misitu,” amesema Profesa Silayo.

Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ni sehemu ya maelekezo mahususi ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo yanataka kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa nchini.

“Sisi kama wasaidizi wake ni wajibu wetu kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa kikamilifu, hususan katika taasisi zenye wanafunzi zaidi ya 100,” amesisitiza Profesa Silayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Mrosso amesema Shule ya Mashati yenye jumla ya wanafunzi 712, inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya Tehama vya kufundishia na kujifunzia.

“Pamoja na maendeleo tuliyonayo, shule yetu ina kompyuta saba pekee, jambo linalofanya tushindwe kufundisha masomo ya Tehama kwa ufanisi,” amesema Mrosso.

Aidha, ameongeza kuwa baadhi ya madarasa ni chakavu kutokana na ujenzi wa muda mrefu, hali inayowalazimu wanafunzi kusoma katika mazingira magumu, hasa kipindi cha baridi kali kutokana na hali ya hewa ya eneo hilo.

Naye mmoja wa wadau wa maendeleo wa shule hiyo, Venance Mallel amemwomba Profesa Silayo kusaidia kuboresha miundombinu ya shule ili wanafunzi waweze kujifunza katika mazingira bora na salama.