Chongolo asihi wananchi kudumisha amani, atoa ahadi kwa wana – Makambako

Njombe. Mgombea ubunge wa Jimbo la Makambako kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa na watu wanaohamasisha vurugu kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Chongolo ametoa wito huo leo Jumapili Oktoba 12, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za kuwanadi wagombea udiwani wa CCM katika kata za Maguvani, Makambako na Majengo, katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.

Amesema wananchi wanapaswa kutambua na kuthamini amani iliyopo nchini, kwa sababu kuna mataifa mengi ambayo yameshindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na kukosekana kwa amani.

“Kuna baadhi ya mataifa yanayotoa fedha kupitia vyama vya siasa kwa lengo la kuvuruga amani ya Tanzania, ili wapate fursa ya kuitawala nchi yetu na kuchukua rasilimali zetu, hasa madini,” amesema Chongolo.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kusimama imara kulinda na kutetea nchi yao, badala ya kugawanywa na ushawishi kutoka mataifa ya kigeni.

“Wananchi lazima tusimame kuitetea nchi yetu na kuacha kugombanishwa. Tujue tunachokitaka na tusikubali kugeuzwa chambo cha maslahi ya wengine,” amesisitiza Chongolo.

Ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge, atajitahidi kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa Makambako, hususan katika upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Maguvani kupitia CCM, Hanana Mfikwa amesema changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa eneo hilo ni miundombinu duni ya barabara pamoja na upungufu wa miundombinu katika sekta ya elimu.

“Sisi tunaomba barabara ziboreshwe, shule ya sekondari ijengwe, na vijana wapewe ajira ili kuboresha maisha yao,” amesema Mfikwa.

Baadhi ya wananchi wa Makambako, akiwemo Partian Myinga, amesema wanatarajia kupata viongozi watakaojikita katika kutatua changamoto zao, hususan miundombinu ya barabara, maji, na elimu.