Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama cha Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema endapo atachaguliwa kuongoza nchi, moja ya mambo ya awali atakayoyatekeleza ni kulirudishia Jiji la Dar es Salaam hadhi yake.
Mwalimu ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Oktoba 12, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Makuti, Kata ya Magomeni, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Februari 24, 2021, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, aliivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa jiji. Hatua hiyo ilihusisha pia kuchukua mali zilizokuwa zikimilikiwa na jiji hilo.
Wakati huo, Magufuli alieleza kuwa uamuzi huo ulitokana na kasoro kadhaa zikiwemo madiwani wa jiji kutochangia maendeleo licha ya kupokea posho na hivyo fedha hizo kuonekana kama zinapotea bure.
Kwa mujibu wa maelezo yake, aliona ni busara fedha za posho na uendeshaji wa madiwani hao kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kama barabara, akibainisha kuwa mfumo wa majiji kama Mwanza na Dodoma una uwakilishi mdogo wa maeneo maalumu, hivyo Ilala ilionekana kufaa zaidi kuwa jiji.

Mwalimu amesema uamuzi wa kulivunja jiji la Dar es Salaam haukuwa sahihi na kwamba Watanzania wakimpatia ridhaa ya kuongoza nchi Oktoba 29, 2025, atalirejesha jiji hilo hadhi yake.
“Mkinipa kura, jambo la kwanza nitakalofanya ni kulirudisha jiji la Dar es Salaam, kwa sababu majiji yote nchini yana jiji na mameya wao,” amesema.
Ameongeza kuwa atahakikisha Dar es Salaam inarejea katika hadhi yake kama jiji la biashara, si la magulio, akisisitiza kuwa anatamani kulifanya kuwa jiji la fursa kwa kila Mtanzania.
“Nataka Dar es Salaam iwe jiji la biashara lenye fursa kwa kila anayekanyaga hapa. Hii biashara ya magulio siyo hadhi ya jiji letu,” amesema Mwalimu.
Aidha, ameeleza kuwa serikali yake itajikita katika kupambana na ugumu wa maisha, hasa katika kodi, bei za vyakula na bidhaa za ujenzi.
“Naomba mniamini, twende tukabiliane na mambo matatu, ugumu wa maisha kwenye kodi, chakula, na gharama za ujenzi,” amesema.
Akigusia kipato cha watumishi wa umma, Mwalimu ameahidi kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano, kima cha chini cha mshahara hakitapungua Sh800,000, huku akibainisha kuwa lengo lake ni kuona kiwango hicho kikiongezeka zaidi kadri uchumi utakavyokua.
Kuhusu ajira, Mwalimu amesema haungi mkono utamaduni wa vijana kutegemea kazi ya ubashiri yaani kubeti, akieleza kuwa hiyo si ajira bali njia ya kuongeza umasikini.
“Tutazalisha ajira kupitia uzalishaji wa ndani, hususan kupitia kilimo na viwanda,” amesema mgombea huyo wa urais kupitia Chaumma.

Awali, mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Kinondoni, Moza Ally amesema akipewa nafasi ya kuwa mbunge atapambana na changamoto za mikopo ya kausha damu inayowatesa wanawake.
Amesema wanawake wengi wamekuwa wakiahidiwa mikopo lakini huishia kudanganywa, hivyo atahakikisha kunakuwepo na timu ya wanasheria na waandishi wa katiba watakao wasaidia wanawake kuandika madokezo sahihi ya miradi yao.
“Mnitume wanawake wenzangu, mimi naweza kujieleza. Kingereza si tatizo kwangu. Nikichaguliwa nitahakikisha wanawake na vijana wanajikwamua kiuchumi,” amesema Moza.
Ameongeza kuwa licha ya jimbo hilo kuwa la mjini, bado miundombinu yake ni duni, hivyo atapigania maboresho makubwa katika barabara na huduma za kijamii.
Aidha, Moza amehitimisha kwa kusema kuwa idadi kubwa ya wananchi wanaojitokeza kwenye mikutano yao ya kampeni inaonyesha imani kwa chama hicho.
Hivyo ameahidi akisinda kiti hicho ofisi yake itakuwa wazi kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao.