:::::::::::::
Kuelekea uchaguzi Mkuu wa Jumatano ya Oktoba 29, 2025 wa kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Tanzania, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imetoa rai kwa watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaoweza kuwaletea maendeleo na kutetea maslahi ya kundi hilo.
Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro Bw. Christopher Mwakajinga ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya utoaji elimu ya kuwajengea uelewa juu ya masuala ya rushwa yenye kauli mbiu: ‘Kataa Rushwa katika Uchaguzi“ kwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu na mahitaji maalum mkoani Morogoro.
Mwakajinga amesema ushiriki wa makundi ya watu wenye mahitaji maalum katika uchaguzi si hisani bali ni haki yao ya msingi inayotokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wanapaswa kushiriki uchaguzi mkuu kikamilifu bila kuwa na vikwazo vyovyote.
Amesema katiba yetu inatoa fursa kwa watanzania wote ambao wametimiza miaka 18 kuwa na haki ya kushiriki kwenye uongozi wa nchi na imetolewa bila kujali ulemavu wa mtu ,vipato vyao, ,hivyo wanapaswa kuitumia sawa na watanzania wengine wasio na ulemavu.
“ Ni lazima tuwekeane mazingira huru na sawa ili muweze kulitumia zoezi hili la msingi la haki ya kupinga kura,“amesema Mwakajinga .
Nao baadhi ya viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti wamewasihi wenzao wasishawishike na kurubuniwa kuchagua viongozi wa shinikizo la kupewa chochote, bali watumie haki yao kuchagua viongozi wanaowataka ili wawaletee maendeleo yao na Taifa na watakaodumisha amani ya Tanzania.